Na Veronica Mrema
Kijiji hadi kijiji kitafikishiwa elimu
sahihi pamoja na uchunguzi wa awali wa kinasaba cha Siko Seli ili kuibua
wagonjwa mapema, waanze matibabu stahiki ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze.
Hatua hii itachukuliwa kwa sababu bado kuna
dhana nyingi potofu ndani ya jamii dhidi ya ugonjwa huo, ikiaminiwa wanaougua wamerogwa
hivyo hupelekwa katika tiba za jadi badala ya hospitalini.
Hata pale wanapofikishwa hospitalini
wagonjwa huwa katika hali mbaya inayowaweka zaidi katika hatari ya kupoteza
maisha, tofauti na wale waliowahishwa na kupata matibabu vema.
Mkoa wa Pwani una jumla ya wagonjwa 5,423
wa Siko Seli, kati yao 1,300 wanaishi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ikifuatiwa
na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze yenye wagonjwa 399.
Takwimu hii ni kwa mujibu wa Ofisi ya Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Pwani na zimetajwa katika kilele cha Maadhimisho ya Mwezi wa
Kujenga Uelewa kuhusu Siko Seli, Mkoa wa Pwani.
Tukio hilo liliandaliwa na Jumuiya ya Watu
Wanaoishi na Siko Seli Tanzania [SCDPCT] kwa ushirikiano na Ofisi ya Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Pwani na wadau mbalimbali, limefanyika Kituo cha Afya Kiwangwa.
“Wengi wanafikiria ni ugonjwa wa kurogwa na
wanachelewa kufika hospitali kupata matibabu, lakini si wa kurogwa unatokana na
urithi wa kinasaba,”.
Mratibu wa Magonjwa Yasiyoambukiza katika
Mkoa wa Pwani Dkt. Eligreater Mzava amesema hayo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Ukio Kusirye, katika kilele cha maadhimisho hayo.
Amesisitiza “Tunahimiza wazazi walete Watoto
[hospitalini], jambo jingine kabla ya ndoa watu wapime, unapopima unakuwa
umejiandaa kisaikolojia.
“Tumemsikia mlezi hapa [mtoto mwenye Siko
Seli] mama [wa mtoto] hakujiandaa, baba naye kakimbia, mama amepata ‘strock’.
“Bibi amelazimika kuchukua jukumu la malezi,
lakini wangejiandaa kisaikolojia, wangelipokea na mtoto angekuwa vema.
Dkt. Mzava ameongeza “Wenye Tatizo wasiogope
waende hospitalini, kuna dawa zinasaidia kupunguza maumivu na mkoa sasa tuna
daktari bingwa wa siko seli.
“.., na pale kwenye uhitaji tutafanya huduma mkoba angalau kwa mwezi awe anatembelea hosptali moja moja aweze kuona hao Watoto,”.
Pamoja na hayo, akimwakilisha Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa
Chalinze Ridhiwani Kikwete,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Chalinze Leon Mgweno amemuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo kuandaa utaratibu
mzuri utakaowezesha wataalamu wake kwenda kuibua wagonjwa hadi vijijini.
“Ambao wamegundulika Chalinze yetu ni 399,
Mkurugenzi na DMO nakuagiza, hii ubainishaji au vipimo, andaa utaratibu mzuri.
“Halmashauri yetu inajimudu kusema kwamba
kila wiki mbili tukatenga siku tatu, tatu kwa kila kata tukawasogezee wananchi huu.
“Wakaenda wakapata uchunguzi na wakapata
majibu, sisi Chalinze tunaweza. Andaa utaratibu, wasiliana na timu ya Wizar ana
Mkoa,” ameagiza.
Mgweno amesisitiza “Kama kunahitaji
uwezeshaji mimi kama Mwenyekiti… tunajimudu, nitafanya hilo kuhakikisha huduma
inafika huko [kwa wananchi], ili tuweze kujipanga tutambue ukubwa wa Tatizo.
“Yaweza ikawa watu huko pengine … kwa
sababu siko seli ni ugonjwa anakuwa na upungufu wa damu, tukaamini mambo ya
kishirikina huko vijijini kwamba sasa ita lambalamba [mganga wa jadi].
“.., ita sijui nani kuna kitu kinakula
mtoto damu. Kuna kitu sijui kinafanya hivi na mambo mengineyo.
“Kumbe ni suala tu la kupima na kujua basi
maisha mengine yanaendelea kama kawaida. Dada yangu pale ukimuona anavyoshine
yupo vizuri kabisa.
“Lakini mtu akisikia siko seli anaona sijui
ni kitu cha aina gani, kumbe ni magonjwa ambayo wewe unaweza ukawa huna siko
seli una magonjwa mengine, hivyo ni vitu vya kawaida kabisa,” amesema.
Amesema Serikali imeendelea kuwekeza ujenzi
wa vituo vya afya vya kisasa kikiwamo cha Kiwangwa pamoja na kuipatia vifaa vya
kisasa vya uchunguzi Halmashauri hiyo.
Kwa muktadha huo nayo itaendelea kuimarisha
huduma kwa kufikia wananchi zaidi ikiwamo huduma hizo za uchunguzi wa awali,
ili kuibua mapema wagonjwa wapate tiba stahiki na waishi maisha bora.
Awali, Diwani wa Kata ya Kiwangwa Malota
Kwaga amehimiza uongozi wa Kituo cha Afya Kiwangwa kuhakikisha kinakusanya na
kuweka data zake vizuri za wagonjwa wa Siko Seli.
“Napongeza ujumbe mliouweka kwenye
maadhimisho haya usemao ‘KUWA MJANJA IJUE SIKO SELI’ na sisi tunashukuru Rais
Samia Suluhu Hassan ametujengea kituo hiki.
“Wananchi wanakuja hapa na kupata huduma
kwa ubora, tunashukuru nanyi mmetuletea maadhimisho haya na wananchi wanapata
elimu sahihi kuhusu Siko Seli, uchunguzi wa afya zao pia,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa SCDPCT Arafa said
amesema lengo hasa ilikuwa kueneza elimu ya Siko Seli pamoja na watu kujijua
hali zao za vinasaba.
“Pia, wananchi wamepatiwa elimu ya lishe,
wamechunguza kisukari, shinikizo la damu, urefu na uzito na kuna waliojitokeza
kuchangia damu kwa hiyari.
“Tunakusudia pia kupata gazelle machine
moja ambayo tutakuja kuileta hapa Kituo cha Afya Kiwangwa ili kuendelea
kushirikiana vema na Serikali kusogeza huduma kwa wananchi.
“Hivyo, tunaendelea kuwaomba wadau mbalimbali
wa maendeleo Waziri watuunge mkono katika hili,” amesema.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Theopister Joseph ameishukuru SCDPCT kwa kuandaa tukio hilo kwani limekuwa lenye
manufaa kwa jamii.
Amemuhakikishia Mgeni rasmi kwamba pamoja na watendaji wa ofisi yake watakwenda kuandaa mpango alioutaka wa kufika kwa jamii kufanya uchunguzi na uelimishaji wa Siko Seli.
Mratibu wa Siko Seli kutoka Wizara ya Afya
Dkt. Asteria Mpoto amesema Tanzania ipo nafasi ya tatu Barani Afrika na ya nne
Duniani kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa Siko Seli.
“Tuna Watoto 14,000 wanaozaliwa kila mwaka
wakiwa na ugonjwa wa Siko Seli, Wizara tunaendelea kuimarisha huduma, hospitali
zote za Rufaa za mIkoa na halmashauri zina kliniki ya Siko Seli sasa.
“Tunaendelea kufikia makundi mbalimbali ya
jamii kuyaelimisha, Siko Seli bado ni Tatizo kubwa, hatutachoka kuendelea kutoa
elimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
“Kuhakikisha huduma zinafika mpaka vituo vya afya na zahanati, maadhimisho ya Kitaifa yanatarajiwa kufanyika Geita,” amesema.

Chapisha Maoni