moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Si kundi kubwa la wanawake ambao huchukua hatua ya kuchunguza mapema hali zao kujua kundi lao la damu ni lipi, kabla ya kuanza mahusiano na kuamua kubeba ujauzito, nchini Tanzania.

Mimba za 'suprize' ndani ya jamii ni suala linaloonekana kuzoeleka, lakini si jema sana kwa afya ya kiumbe tarajiwa kilichopo tumboni mwa mama.

Kwa sababu kuna ambao hupoteza ujauzito kwa sababu ya kundi lao la damu, lakini ikiwa angejua hilo mapema, basi angeshauriwa vema na kuchukua hatua mapema kuokoa kizazi chake.

Je, kundi langu la damu ni lipi? Ni swali ambalo kila mwanamke anapaswa kujiuliza na kuchukua hatua ya kufika vituo vya kutolea huduma za afya ili akachunguzwe na kujua mapema.

Maandalizi ya mapema huokoa maisha ya kiumbe tarajiwa mapema, amesisitiza Meneja Mpango wa Taifa wa Damu Salama Tanzania, Kanda ya Mashariki [EZBTS] Dkt. Pendael Sifueli.

Ni katika viwanja vya Mbagala alipokuwa akishiriki Wiki ya Taasisi ya JAI ambayo imeambatana na uhamasishaji jamii kuchunguza afya pamoja na kuchangia damu.

"Mojawapo ya fursa ambazo mtu anaweza kupata kupitia uchangiaji damu ni kufahamu hali yake ya afya, kupata ushauri wa wataalamu na pia kujua kundi lake la damu,' amesema.

Ameongeza "Ukichangia damu unapata faida kubwa tatu, moja unakuwa unajua hali yako ya afya, pili unakuwa shujaa kwa sababu unasaidia kuokoa maisha ya mtu mwingine.

"Tatu, unapewa ushauri wa afya na wataalamu wetu na itakusaidia kuendelea kuwa imara kwani utaitunza, kwani itakusaidia kuwa na mwenendo mzuri wa kimaisha.

"Kwa wanawake, anasema kufahamu kundi la damu mapema kuna umuhimu wa pekee, hasa kabla ya ujauzito.

Dkt. Sifuel amesisitiza mwanamke ambaye bado hajapata ujauzito akifahamu kundi lake la damu mapema anaweza kupata ushauri wa wataalamu kuhusu hali yake.

“Ushauri utamsaidia kufanya maamuzi na chaguo sahihi, kwani kuna hatari za kupoteza mimba ya kwanza usipojua kundi lako la damu.”

Kauli hiyo inaibua umuhimu wa wanawake kuwa na mwamko wa kufahamu taarifa zao za afya kabla ya ujauzito, badala ya kusubiri hadi wanapokuwa tayari wajawazito ndipo waanze kuzitafuta.

Pamoja na hayo, wanawake wamehimizwa kujitokeza kuchangia damu kwa hiyari, kwani licha ya kuwa miongoni mwa wahitaji wakubwa hasa kipindi cha kujifungua bado wapo nyuma kujitolea kwa hiyari.

Kwa hiyo, mwanamke anayejua kundi lake la damu na taarifa nyingine muhimu za afya yake si tu anajiandaa kwa safari yake ya afya, bali anaweza pia kuwa sehemu ya kuhakikisha mwanamke mwingine anayefika hospitalini akiwa na uhitaji wa damu anapata msaada.

"Uhitaji wa damu ni mkubwa na mahitaji yanaongezeka kila siku kila siku kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, kukua kwa maendeleo na ajali za barabarani,".

Dkt. Pendael amesisitiza "Tanzania sasa ina huduma za upasuaji wa kibingwa ambazo miaka ya nyuma hazikuwapo nchini, huku zikiwemo oparesheni kubwa kama za moyo.

"Kuna huduma za upasuaji wa kibingwa pia ambazo miaka ya zamani hazikuwapo nchini lakini sasa zinafanyika oparesheni kubwa kama moyo nakadhalika.”.

Tanzania pia inapokea wagonjwa kutoka nje ya nchi wanaokuja kutibiwa nchini, hali inayoongeza umuhimu wa kuhakikisha huduma bora na upatikanaji wa damu kwa wanaohitaji.

"Sasa tunapokea pia wagonjwa kutoka nje ya nchi wanakuja kutibiwa Tanzania, na Serikali lazima ihakikishe wanapata huduma bora. 

"Kwa mantiki hiyo lazima tutafute damu ili kuokoa maisha ya wahitaji." amesema.

Mgeni rasmi katika zoezi hilo, Dkt. Timoth Bende, kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Temeke, amesema uchangiaji damu ni tendo la huduma na upendo, akisisitiza kuwa hakuna anayejua ni lini yeye mwenyewe au mtu wake wa karibu anaweza kuhitaji damu.

“Uchangiaji damu ni tendo kubwa la huduma na upendo. Kuna umuhimu mkubwa tunaokoa maisha ya wengine,” amesema.

Amesema mtu anaweza kuchangia damu leo na kesho damu hiyo ikawa msaada kwake, ndugu, jamaa, jirani au rafiki.

“Tunatembea hakuna anayejua kesho, unaweza ukatoa damu leo na kesho ikakusaidia kama si wewe, basi ndugu, jamaa, jirani au rafiki yako.”

Ametaja wajawazito, watoto, majeruhi, wanaopata ajali na watu wenye changamoto za kiafya kama Siko Seli, kuwa miongoni mwa wanaoweza kuhitaji damu.

"Nani wa kuwaokoa ni sisi wenyewe wananchi kwa ushirikiano na wataalamu wetu wa afya, tujitokeze kuchangia damu na Mwenyezi Mungu atajalia.”.

Hakuna maabara wala kiwanda kinachoweza kutengeneza damu kwa ajili ya kuokoa uhai wa binadamu, bali damu hutegemea mtu anayeguswa na kujitolea kuchangia kwa hiari.

Ametoa pongezi kwa JAI kwa kujitolea kwa jamii na kwamba hatua hiyo inakwenda kusaidia kuokoa uhai wa watu wengi..

Wananchi hawakupewa nafasi ya kuchangia damu pekee, bali pia walipata huduma za uchunguzi wa afya ikiwemo Siko Seli, malaria, TB, shinikizo la damu, kisukari na UKIMWI na ushauri wa afya.

Amir wa JAI amesema zoezi hilo ni mwendelezo wa maadhimisho ya Wiki ya JAI Tanzania ambayo yanafanyika katika mikoa mingine nchini.

"Wanachama wetu wanapata nafasi ya kujitokeza kupata huduma, pamoja na wananchi wengine sisi hatubagui dini, sote ni wamoja, katika kusaidia jamii," amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bone and Blood Foundation, Neema Mohamed, amesema taasisi hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 2021 imekuwa ikishirikiana na jamii kukusanya damu.

Amesema pia imekuwa ikiungana na taasisi nyingine, ikiwamo JAI, kupanua wigo wa huduma hizo.

"Hapa leo tunafanya uchunguzi wa awali wa kinasaba cha Siko Seli na kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo, bila malipo," amesema.

Daktari Rhoby Jeremiah amesema wagonjwa wa Siko Seli hukumbana na changamoto nyingi kila siku ya maisha yao.

Amesema wengi wao hutibiwa kulingana na dalili wanazokuwa nazo wakati wanapitia maumivu, ikiwemo yale makali yanayojulikana kama crisis.

“Ikiwa damu amepunguzwa anaongezwa, au anapewa vidonge kumsaidia. Tiba ipo lakini ni gharama kubwa, mgonjwa mmoja anahitaji TZS Mil. 70 na zaidi ili kupata tiba ya upandikizaji Uloto.”

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani [WHO] Tanzania ipo miongoni mwa nchi tatu zenye idadi kubwa ya wagonjwa wa Siko Seli Barani Afrika na ni ya nne duniani.

Dkt. Rhoby amedokeza "Kila mwaka kati ya 11%-17% ya watoto huzaliwa na ugonjwa wa Siko Seli, na huchangia 7% ya vifo vya watoto wachanga kila mwaka, nchini.

"Ndani ya jamii kuna kati ya 17%-20%  ya watu ambao bado hawajijui kuwa wamebeba vinasaba vya ugonjwa huo.

"Yaani kati ya watu 10 unaweza kukuta wawili wana vinasaba vya ugonjwa na hawajijui maana yake hawa wakioana wanaendeleza ule mduara wa ugonjwa.”

"Ndiyo maana, anasema, jamii inapaswa kufikiwa kwa elimu na uchunguzi ili watu wafahamu hali zao mapema.

“Ndiyo maana tunakuja kwa jamii kuwapima, wajijue hali zao, tunawaelimisha waielewe Siko Seli ili wavunje mduara wa ugonjwa huu na tuweze kuokoa maisha.” amesisitiza Dkt. Rhoby.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement