Na Veronica Mrema
Visa vya watoto kujiua vinarekodiwa ndani ya jamii, lakini kwa wengi wetu kila taarifa kama hiyo huacha maswali mazito.
Mtoto? Kajiua? Kulikoni? Kwa nini? Kwa nini mtoto ambaye maisha yake ndiyo kwanza yameanza afikie hatua ya kusitisha uhai wake?
Kwa nini mtoto anayetarajiwa kuwa shuleni, kucheza, kujifunza na kuota kuhusu maisha yake ya baadaye afikie mahali pa kuona kwamba hakuna sababu tena ya kuendelea kuishi?
Na zaidi ya yote, ni nini kilikuwa kinaendelea ndani ya maisha yake kabla hajafikia hatua hiyo?
Ni maswali yanayohitaji kuanza kujadiliwa mapema na kuchukua hatua stahiki, kabla ya jamii kulazimika kuyauliza baada ya mtoto kupoteza maisha.
Agosti Mosi, 2026, Muslimah Medical Support Fund (MMSF) iliwakutanisha wataalamu wa afya na wadau mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Mkutano uliobeba kaulimbiu “Caring for Today, Building a Healthier Tomorrow”, ukilenga kujadili namna ya kuimarisha afya na ustawi wa jamii.
Miongoni mwa masuala yaliyopewa uzito ni afya ya akili, hususan changamoto zinazowakabili watoto na vijana.
Mwanasaikolojia Saldeen Kimangale anasema watoto pia hukabiliwa na changamoto za afya ya akili na kwamba kuna umuhimu mkubwa kwa jamii kuanza kuwaangalia kabla changamoto haijafikia hatua ya mwisho.
Kimangale anasema swali la “kwa nini mtoto?” linapaswa kutusukuma kutafuta kilichokuwa nyuma ya tukio hilo, mazingira ambayo mtoto alikuwa akiishi.
Changamoto alizopitia, namna alivyolelewa na kama kulikuwa na ishara za mapema ambazo zingeweza kuonekana.
SWALI LA DUNIA
Tanzania si peke yake inayokabiliwa na changamoto hii ya watu kujikatisha uhai ikiwamo kundi la watoto.
Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu 720,000 hufa kwa kujiua kila mwaka duniani, huku kujiua kukiwa miongoni mwa sababu kuu za vifo kwa vijana.
WHO inaeleza kwamba mwaka 2021 kujiua kulikuwa sababu ya tatu ya vifo kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 29 duniani, huku asilimia 73 ya vifo hivyo vikitokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.
Kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 19, WHO inasema kujiua ni miongoni mwa sababu kuu za vifo.
Lakini nyuma ya takwimu za vifo kuna tatizo kubwa zaidi ambalo huanza mapema.
WHO inakadiria kwamba mtu mmoja kati ya kila watu saba wenye umri wa miaka 10 hadi 19 duniani anaishi na tatizo la afya ya akili.
“Hii ina maana kwamba tunapozungumzia afya ya akili ya watoto na vijana, hatuzungumzii kundi dogo la watu,” anasema Kimangale.
“Tunazungumzia kizazi na tunazungumzia changamoto ambazo zinaweza kuanza kabla mtoto hajafikia hata balehe.”
WHO inaeleza kwamba hadi nusu ya matatizo ya afya ya akili huanza kabla ya umri wa miaka 14, huku nusu ya matatizo ya afya ya akili ya watu wazima ikiwa imeanza kabla ya miaka 18.
Tatizo ni kwamba visa vingi havitambuliwi wala kutibiwa mapema.
Kwa hiyo, mtoto anayefikisha miaka 15, 16 au 17 akiwa na changamoto kubwa ya afya ya akili huenda tatizo hilo halikuanza siku aliyofikia umri huo.
Huenda lilianza miaka kadhaa iliyopita nyumbani, shuleni, katika mahusiano yake na wazazi au walezi, katika ukatili aliowahi kupitia, kunyanyaswa, kukataliwa au kutengwa, au katika maumivu ambayo hakuwahi kupata mtu wa kuyasikiliza.
KWA NINI MTOTO?
Kimangale anasema swali hili limekuwa na uzito zaidi kwake kutokana na taarifa anazokusanya binafsi kuhusu watoto wanaojiua nchini Tanzania tangu mwaka 2019.
Anasema hadi Juni mwaka huu, watoto 18 wenye umri kati ya miaka 10 na 15 walikuwa wamesitisha maisha yao.
“Hivi ninavyozungumza hata wiki haijaisha kuna mtoto amesitisha uhai wake. Unajiuliza kwa nini mtoto? Kwa nini mtoto?” anasema.
Kwa Kimangale, nyuma ya kila mtoto anayepoteza maisha kuna uwezekano wa kuwa na historia ambayo jamii haikuisoma kwa wakati.
Ndiyo maana hatupaswi kuanza kuuliza maswali siku mtoto anapokufa. Tunapaswa kuanza wakati bado yupo hai.
RIKA, JINSIA AU DINI?
Suala la changamoto, matatizo au magonjwa ya akili halichagui dini, jinsia wala rika, anasisitiza Kimangale.
“Mojawapo ya dhana ambazo jamii inapaswa kuziacha ni kwamba ugonjwa wa akili ni wa kundi fulani la watu.
“Magonjwa ya akili hayana umaalum baina ya mwanamke au mwanaume, mtoto au mkubwa, Muislamu au asiye Muislamu. Yeyote yupo kwenye hatari ya kupata changamoto ya afya ya akili,” anasema.
Anaongeza “Mtu anaweza kupata changamoto ya afya ya akili bila kujali kiwango chake cha imani. Anaweza kuwa Mcha Mungu.
"Anaweza kuwa anaswali. Anaweza kusoma Qur’an. Na bado akahitaji msaada wa kitaalamu.
“Hatuna umaalum kwamba hatuwezi kuugua. La hasha.” Kwa upande mwingine, mtu asiye na sifa hizo za kiimani anaweza asiwe na ugonjwa wa akili.
Hivyo, afya ya akili haiwezi kupimwa kwa kiwango cha mtu cha ibada
IMANI NA TAALUMA
Kwa Kimangale, mtoa huduma wa afya anabeba dhamana mbili; kumwakilisha Mwenyezi Mungu kwa uadilifu na wakati huo huo kusimama katika taaluma.
“Duniani tumebeba dhamana. Moja, tumwakilishe Mwenyezi Mungu, lakini kwa upande mwingine tusimame katika professionalism,” anasema.
Anatumia simulizi ya Nabii Yusuf na baba yake, Nabii Yaqub, kueleza kwamba kuwa mtu wa imani hakumaanishi mwanadamu hawezi kupitia maumivu makubwa ya kihisia.
Baada ya Yusuf kutoweka na ndugu zake kumweleza baba yao kwamba ameliwa na mbwa mwitu, Yaqub alipata huzuni kubwa na kuendelea kumlilia mwanawe mpaka uoni wake ukapotea.
Kwa mtazamo wa leo, anasema Kimangale, mtu anayepitia hali kama hiyo angehitaji pia kutathminiwa kiafya.
Hii haimaanishi kupunguza nafasi ya imani. Badala yake, ni kutambua kwamba maumivu ya kisaikolojia yanaweza kumpata hata mtu mwenye imani kubwa.
TATIZO JINGINE
Kimangale anataja pia namna jamii inavyotafsiri ugonjwa wa akili.
Anasema baadhi ya watu wanapopata changamoto hizo huanza kwa waganga wa kienyeji, huku wengine baadaye wakiwafuata viongozi wa dini.
Kwa baadhi ya waumini, changamoto hiyo inaweza kutafsiriwa kama udhaifu wa imani.
Mtu anaweza kuambiwa aswali zaidi, afanye udhu au asome Qur’an, huku bila kupata tathmini ya kitaalamu.
Kimangale hasemi msaada wa kiroho hauna nafasi. Anachosisitiza ni kwamba msaada wa kiroho haupaswi kuchukua nafasi ya matibabu ya kitaalamu pale mtu anapohitaji huduma ya afya ya akili.
Kwa sababu mtu anaweza kuwa na imani na wakati huo huo akawa mgonjwa.
Aidha, katika jamii, mtu mwenye ugonjwa wa akili wakati mwingine hupewa majina kabla hajapewa huduma.
“Akiwa anazungumza mwenyewe, anaweza kusemwa amerogwa. Akiwa amebadilika tabia, anaweza kuambiwa amelaniwa. Akiwa mkali, anaweza kuonekana kama mtu mbaya. Wengine huishia kuachwa mitaani,” anasema.
Kimangale anamtaja mwanahisabati maarufu John Nash, ambaye aliishi na schizophrenia kwa miaka mingi lakini akaendelea kutambulika duniani kwa mchango wake mkubwa katika taaluma yake.
Ujumbe wake ni kwamba ugonjwa wa akili hauondoi uwezo wa mtu. “Wakipata matibabu sawa sawa wana uwezo wa kupona na wakarudi kawaida kuendelea na maisha yao,” anasema.
Hivyo, mtu anayepitia ugonjwa wa akili anahitaji huduma, si hukumu.
MTOTO TUNAYEMUITA MTUKUTU
Mjadala huu unakuwa muhimu zaidi unapowahusu watoto. Mtoto anapobadilika tabia, jamii inaweza kumuita mtukutu, mkorofi au asiye na adabu.
Kimangale anasema hata baadhi ya makundi ya vijana yanayoonekana mitaani kama “wahuni” yanapaswa kuangaliwa kwa jicho la afya ya akili., bila kumaanisha kwamba kila mtoto mwenye tabia hiyo ana ugonjwa wa akili.
Dar es Salaam tumewahi kushuhudia makundi kama Panya Road, huku katika mikoa mingine vijana wakitumia majina tofauti kujitambulisha.
Lakini kabla ya kuishia kusema “hawa ni wahuni”, Kimangale anataka jamii iulize, kuna nini kiliharibika katika ufahamu wao?
Mtoto anayechukuliwa kwa sababu ya tabia yake na kupelekwa katika mazingira yenye ukatili zaidi huenda tatizo lisitatuliwe. Linaweza kuongezeka.
UKATILI WA UTOTONI TUNAOZOEA
Hapa ndipo hoja ya 'early childhood adversities' inapokuwa muhimu.
“Mtoto anaweza kupigwa. Kutukanwa. Kukataliwa. Kutengwa. Kudhalilishwa. Kunyanyaswa. Au kukulia katika mazingira yenye migogoro na hofu.
“Baadhi ya mambo haya yamezoeleka kiasi kwamba jamii imeanza kuyaona kama sehemu ya kawaida ya malezi.
“Lakini kwa mtoto, uzoefu huo unaweza kuwa na athari kubwa katika ukuaji wake wa kihisia na kisaikolojia,” anasema Kimangale.
WHO inaeleza kwamba mazingira kama ukatili, umaskini, kutengwa na ubaguzi yanaweza kuongeza hatari ya vijana kupata changamoto za afya ya akili.
Kimangale anasema baadhi ya uzoefu huo unaweza kuathiri uwezo wa ubongo wa mtoto kudhibiti hisia.
Hivyo, mtoto anayeshindwa kudhibiti hasira, huzuni au hofu si lazima awe “mtoto mbaya”. Huenda kuna jambo analobeba.
Tunataka kuwasaidia watu, lakini wakati mwingine tunawaacha watoto. Hata watu wazima wanapaswa kujiuliza kuhusu mazingira ambayo watoto wao wanakulia.
Kuna mzazi anayesaka elimu zaidi. Mwingine anatafuta utaalamu. Mwingine anahangaika kutafuta fedha. Mtoto anaachwa kwa bibi, ndugu au mlezi mwingine.
Hakuna anayesema mzazi huyo hana nia njema. Lakini mtoto bado anaendelea kukua.
Na katika harakati hizo za kutafuta maisha bora, watu wazima wanaweza bila kukusudia kuwaweka watoto katika mazingira yanayowaathiri.
Mtoto anahitaji uwepo. Anahitaji usalama. Anahitaji mtu wa kumuuliza, “Unaendeleaje?”
MMSF NA MTOTO
Kwa Muslimah Medical Support Fund (MMSF), mjadala huo unaendana na kazi ambayo taasisi hiyo imekuwa ikifanya ya kusaidia watoto kutoka familia zisizo na uwezo kupata huduma za afya.
Mwenyekiti wa MMSF, Dkt. Asha Mahita, anasema mtoto anapokuwa na changamoto ya kiafya, athari zake haziishii kwenye mwili pekee.
Familia nayo inaweza kuingia katika msongo mkubwa wa mawazo kutokana na gharama za matibabu, hofu kuhusu hali ya mtoto na changamoto za maisha ya kila siku.
“Mtoto anapokuwa na changamoto ya kiafya, familia yake nayo inaweza kupitia hali kubwa ya msongo wa mawazo.
“Ndiyo maana tunahitaji kuangalia afya ya mtoto kwa ujumla, si ugonjwa pekee alionao,” anasema Dkt. Mahita.
MMSF imekuwa ikiwasaidia watoto kupata bima ya afya na kugharamia matibabu kwa familia zisizo na uwezo.
Ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha watoto hawakosi huduma kwa sababu ya hali ya kiuchumi ya wazazi wao. Dkt. Mahita anaongeza,
“Tunapozungumzia mtoto, tunapaswa kuangalia afya yake kwa ujumla. Huduma ya afya haipaswi kuishia kwenye kutibu ugonjwa mmoja; tunahitaji pia kuangalia ustawi wake.”
MTOA HUDUMA ANAWEZA KUFANYA ZAIDI YA KUANDIKA DAWA
Hapa ndipo ujumbe wa Kimangale kwa wataalamu wa afya unakuwa muhimu.
Mtoa huduma anayekutana na mtoto katika mazingira ya huduma za afya anaweza kugundua changamoto ambayo haionekani kwenye ugonjwa anaokuja kutibiwa.
Ndiyo maana Kimangale anawataka wataalamu wa afya kujiuliza ni msaada gani mwingine wanaweza kumpa mgonjwa zaidi ya dawa wanazomuandikia.
“Unapokuwa ukimpa huduma mtu, zaidi ya zile dawa unazomuandikia, kipi kingine unaweza kufanya kumsaidia?” anauliza Kimangale.
Kwa mtazamo wake, swali hilo ni muhimu zaidi kwa watoto kwa sababu changamoto wanazopitia zinaweza kuathiri ukuaji wao wa kihisia na kisaikolojia na, zisipotambuliwa mapema, kuendelea hadi ukubwani.
Hapo ndipo maana ya “Caring for Today, Building a Healthier Tomorrow” inapopata uzito wake.
Kumjali mtoto leo si kumtibu ugonjwa anaokuja nao pekee. Ni kuangalia afya yake kwa ujumla, mazingira anayokulia, changamoto anazopitia na ustawi wake wa akili.
Kwa sababu kabla ya kuuliza “kwa nini mtoto?” baada ya kumpoteza, jamii inapaswa kujifunza kumuuliza mtoto akiwa bado hai, “Unaendeleaje?”
Huenda swali hilo dogo likawa mwanzo wa kugundua maumivu ambayo mtoto amekuwa akibeba kimya kimya.
Na huenda hatua hiyo ya mapema ikawa tofauti kati ya mtoto anayepoteza matumaini na mtoto anayepata nafasi ya kuendelea kuishi, kukua na kujenga kesho yenye afya zaidi.

.jpeg)
.jpeg)
Chapisha Maoni