Na Veronica Mrema
Umri wake ni miaka 36 tu, haikuwa jambo jepesi kwake kukubali ukweli kwamba amegundulika ana saratani ya titi na linapaswa kuondolewa ikiwa ni sehemu ya tiba kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
"Siku moja nikiwa bafuni naoga, nilibaini kijiuvimbe kidogo kwenye titi langu moja," anasimulia Betty Mgeni, Mkazi wa Gongo la Mboto, Dar es Salaam.
Awali hakuhofia sana alihisi ni ka-uvimbe ka-waida ambako kangepotea baada ya muda fulani, lakini haikuwa hivyo.
Betty alifika hatua ya kuamua kwenda hospitalini kwa uchunguzi zaidi, "Nilianzia zahanati moja iliyo jirani, walinichunguza na hawakuweza kujua zaidi kilichokuwa kinanisumbua".
Baada ya kuona bado ka-uvimbe kale kapo kwenye titi lake aliamua kuchukua hatua zaidi na kufika Taasisi ya Saratani Ocean Road [ORCI], huko baada ya uchunguzi ilibaini ana saratani ya titi.
Si taarifa nyepesi kwa walio wengi, Betty anasimulia "Nilihisi kama maisha yangu yamefikia mwisho, nilidhani nakufa sasa, baada ya kupewa taarifa hii, nilipata mshtuko.
Alirudi nyumbani, alieleza familia yake kile kilichobainika, mapokeo yalikuwa mseto. "Niliambiwa pole, lakini kuna walioniambia niende kwa mganga na wengine walisema niendelee na tiba hospitalini.
HALI HALISI
Licha ya maendeleo katika huduma za afya, saratani bado ni miongoni mwa changamoto kubwa za afya ya umma nchini Tanzania.
Kundi la wanawake na vijana wanaendelea kubainika kuugua ugonjwa huo nchini Tanzania, hata wale ambao wapo katika umri mdogo, kama ilivyokuwa kwa Betty.
Kwa mujibu wa makadirio ya Shirika la Afya Duniani [WHO] kupitia utafiti wake wa Globocan wa 2022, Tanzania ilikadiriwa kuwa na zaidi ya wagonjwa wapya 44,000 wa saratani kila mwaka.
Vifo vitokanavyo na saratani kila mwaka vinakadiriwa kuwa 29,000, huku saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake na saratani ya tezi dume kwa wanaume zikiongoza kwa idadi ya wagonjwa na vifo.
Ripoti zinaonesha pia kuwa zaidi ya watu 89,000 wanaishi na saratani ndani ya miaka mitano baada ya utambuzi, jambo linaloongeza umuhimu wa huduma za ufuatiliaji wa wagonjwa baada ya matibabu.
SI HUKUMU YA KIFO
Mkurugenzi wa Shujaa Cancer Foundation [SCF], Gloria Kida, amefikisha miaka 16 sasa tangu alipopona saratani ya matiti, anasema jamii bado inahitaji kubadilisha mtazamo kuhusu ugonjwa huo.
SCF imekuwa ikishiriki moja kwa moja katika kuelimisha jamii, Juni 7, mwaka huu iliungana pamoja na mashujaa waliougua na kupona ugonjwa huo kuadhimisha Siku ya Mashujaa wa Saratani Duniani.
Gloria anasema lengo la siku hiyo ni kuwapa wagonjwa matumaini na kuwaonesha kuwa maisha yanaendelea baada ya saratani.
“Watu wengi wanapopata taarifa ya saratani wanafikiri ni mwisho wa maisha, lakini tunawaonesha kuna maisha baada ya matibabu,” anasema.
Anasema hatua ya kukutana kwa walionusurika huongeza uelewa na kuwajenga wagonjwa wapya kisaikolojia.
"Hasa wanapoona watu waliodumu na maisha kwa zaidi ya miaka 10 au 20 baada ya matibabu," anabainisha.
UFUATILIAJI KLINIKI
Sarah Nyagabona ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani Hospitali ya Taifa Muhimbili [MNH] anasema kuna umuhimu mkubwa kwa anayekabiliana na satarani kuzingatia kliniki.
Ni hatua ya msingi inayosaidia kwanza ugunduzi wa mapema, ufuatiliaji wa mwenendo wa hali ya mgonjwa pia.
"Hata kama kuna hatari ya uwezekano wa ugonjwa kujirudia, kwa wale ambao walitibiwa na kupona inakuwa rahisi kugundua mapema na kuchukua hatua," anasema.
Dkt. Nyagabona ameongeza "Saratani ina tabia ya kukua na kusambaa iwapo haitafuatiliwa kwa karibu.
"Hivyo wagonjwa wanapaswa kuendelea na ratiba za kliniki hata baada ya kuonekana kupona.
“Madaktari ni washirika wa wagonjwa. Wagonjwa wanapaswa kuwa huru kueleza changamoto zao ili tuweze kuwasaidia,” anasema.
Ufuatiliaji huu, unaojulikana kitaalamu kama 'Surveillance', ni sehemu muhimu ya kuhakikisha maisha bora baada ya matibabu.
CHANGAMOTO
Gharama za matibabu bado zinatajwa ni mzigo kwa walio wengi katika kupambana na saratani.
"2013 niligundulika na saratani ya titi upande wa kushoto, nikatibiwa, liliondolewa, nikapata tiba ya kemia na miondiz, nikapona," anasema Tusekalunde Kasitu.
Baada ya miaka 11 [mwaka 2025] amebainika tena na viashiria uvimbe titi la pili nikatibiwa na kuondolewa nimefanya kemo nimemaliza na sasa nipo kwenye mionzi.
Anasema kilio kikubwa kwa wagonjwa wa saratani ni gharama za matibabu, hasa kwa wale waliokata vifurushi vya Bima ya Afya ya Taifa, kuna baadhi ya huduma hazipatikani.
"Tunaambiwa tukate bima, tunakata lakini matibabu ni makubwa sana, kwa upande wangu siwezi kumshauri mtu wa saratani akate bima ya kifurushi.
"Inatesa kwa sababu unakuta umepata bima kwa kuchangiwa, unaanza kupata matibabu kisha unalazimika kurudi tena kwa wale wale waliokuchangia, wakuchangie tena," anasema.
Anaongeza "Mpaka wanakuuliza mbona tulikuchangia umepata bima, inakuwaje unataka tena kuchangiwa, wao wanasema bima kama matibabu mil. 3 utachangia mil. 1.5.
"Kitu ambacho mimi na familia tulishaelekezwa ukiwa na bima itakuwa free kumbe ndiyo unaongeza gharama.
"Mfano mionzi kwa mtu wa kawaida [asiye na bima, wanaita'cash sharing'] anatakiwa kulipia 100,000 mionzi 25, lakini wewe mwenye kifurushi unaambiwa Mil 2.5 bima inakulipia nusu.
"Kwa hiyo Mil. 1.5 unalipia wewe, kitu ambacho kwa familia za kawaida ni ngumu," anasema hivyo wanaomba Serikali itazame upya suala hilo na kuwapunguzia mzigo wa gharama.
Pamoja na hayo, Tanzania kupitia Wizara ya Afya kwa ushirikiano na wadau wengine wa maendeleo imepanua wigo wa uchunguzi wa awali wa saratani mbalimbali na matibabu.
Serikali pia imetangaza dhamira ya kupunguza vifo vya saratani kwa zaidi ya asilimia 30 katika miaka ijayo kupitia mikakati ya kitaifa ya udhibiti wa saratani.
Ingawa saratani bado ni tishio kubwa nchini Tanzania, ushuhuda wa mashujaa unaonesha wazi kuwa ugonjwa huo si hukumu ya kifo.
Ufunguo mkubwa unaobaki ni uchunguzi wa mapema, ufuatiliaji wa kliniki, na elimu kwa jamii, hasa kwa vijana na wanawake wanaoanza kugundua dalili katika umri mdogo.
Betty alichagua kuendelea na matibabu hospitalini na sasa anafurahia mwenendo wa hali yake.
"Niliondolewa titi, sasa maendeleo yangu ya afya ni mazuri, nimeimarika na ni vigumu mtu kujua kwamba ninakabiliana na saratani, labda nimwambie mimi mwenyewe," anasema.
Anaongeza “Nawashauri wanawake na mabinti wajichunguze mapema na waende hospitali mara wanapohisi dalili zisizo za kawaida".

Chapisha Maoni