moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Bidhaa za sigara mbadala [zisizotoa moshi] hivi karibuni zilijadiliwa kwa kina na mapana na watafiti nguuli, wanasayansi, Wanahabari na watunga sera Barani Afrika, walipokutana Afrika Kusini.

Ni katika mkutano mahususi ulioandaliwa na PMI uliobeba agenda TECHNOVATION [Smoke-Free] 2025 watafiti wakidai bidhaa hizo zinalenga kusaidia jamii kwa kupunguza madhara ya kiafya kwa watumiaji na watu wanaokuwa karibu na watumiaji.

Hivyo, mkutano huo uliwaleta pamoja makundi hayo huko Jijini Johannesburg, Afrika Kusini kuangazia bidhaa hizo ambazo kwa nchi nyingi sasa soko lake linashika kasi kubwa.

Mataifa kadhaa tayari yameweka sera na miongozo ya wazi ya usimamizi, huku mengine yakibaki kimya yakisubiri tafiti na mjadala mpana wa kitaifa.

Hali hii imeibua hoja muhimu kwa Tanzania je, Taifa hili lililopo Ukanda wa Afrika Mashariki Sheria na mifumo yake ya udhibiti iliyonayo inatosha? 

Hasa ikizingatiwa kwamba hivi sasa inaendelea kushuhuia ongezeko la vijana wanaogeukia matumizi ya bidhaa hizi mbadala katika kumbi mbalimbali za starehe na mitaa kadhaa ndani ya jamii yake.

Kwa Tanzania, jukumu la udhibiti wa bidhaa zitokanazo na tumbaku lipo chini ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba [TMDA] tangu mwaka 2021. 

Lakini bado Sheria ya Tumbaku ya mwaka 2003 haijataja wazi namna ya kudhibiti bidhaa mpya kaka e-cigarettes na shisha.

Jambo linaloacha pengo la kisheria katika wakati ambapo matumizi yake yanaendelea kuongezeka sokoni.

Ili kupata majibu, M24 TANZANIA MEDIA imefanya mahojiano maalum na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo.

Dkt. Fimbo ndani ya makala haya anaeleza kwa undani hali ya udhibiti, changamoto na mwelekeo wa Tanzania katika kulinda afya ya jamii dhidi ya bidhaa hizi.

M24 TANZANIA:  Je, TMDA ina wajibu gani hasa katika kusimamia bidhaa za tumbaku zinazounzwa nchini hasa katika udhibiti wa ubora wake ili kulinda afya ya jamii, nchini Tanzania? 

TMDA: Tulikasimiwa jukumu la kudhibiti bidhaa za tumbaku kupitia tangazo la Serikali mwaka 2021 ambalo lilipitishwa na Waziri wa Afya, kazi yetu kubwa ni kufanya udhibiti wa bidhaa za [tumbaku].

Kwa maana ya kuorodhesha bidhaa zote za tumbaku ambazo zinatengenezwa Tanzania, kufanya uukaguzi wa soko ili kuhakikisha bidhaa zile ambazo zimeorodheshwa ndizo ambazo zinapatikana kwenye soko, pia kufanya ufuatiliaji wa madhara yoyote ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na matumizi ya bidhaa za tumbaku. 

Katika bidhaa za tumbaku kuna kemikali kama 92 ambazo zina madhara makubwa kwenye miili ya binadamu na kemikali hizo ndizo ambazo sisi tunazifuatilia ili kuhakikisha bidhaa zote za tumbaku hazina kemikali hizo. Ukiangalia kwa mfano bidhaa nyingi za tumbaku zina nikotini. ni bidhaa kubwa ambayo ipo kwenye bidhaa za tumbaku na ndiyo ambayo inayoleta ulevi kwa watumiaji.

Unakuta kuna [watengenezaji] wengine ambao wanaongeza kile kiasi cha nikotini kwenye bidhaa hizo, kwa hiyo jukumu letu kubwa sisi ni kuhakikisha kwamba kiasi hicho [cha nikotini] hakiongezeki nje ya kiwango ambacho kimewekwa ili kisiweze kudhuru watumiaji.

Ndiyo kazi kubwa tunayoifanya, pia kuangalia maeneo ambayo bidhaa za tumbaku zinavutwa kwa maana [kwamba], kama ni maeneo ya wazi labda maeneo ya staree, baa, migawaha waweze kutenga maeneo kwa ajili ya kuruhusu wavuta tumbaku, wavute [pamoja], ale ambao hawavuti wasidhurike na ule moshi wa tumbaku, kwa sababu ule moshi kwa mtu ambaye havuti akiwa karibu na mvutaji unamuathiri, kwa hiyo ndiyo maeneo makubwa tunasimamia na kuyafanyia kazi.

M24 TANZANIA:  Je, unaweza sasa kunifafanulia Sheria au miongozo gani inatumika katika udhibiti wa bidhaa hizi?    

TMDA: Katika udhibiti wa bidhaa hizi, kuna Sheria ya tumbaku, ya mwaka 2003 ambayo ilitungwa na bunge, imeweka masharti ya utaratibu mzima wa kusimamia sekta nzima ya bidhaa za tumbaku. kuna sheria nyingine inahamasisha kilimo, hiyo haihusiki na TMDA ni wenzetu wa Wizara ya Kilimo wanahamasisha zao la tumbaku, ulimaji wa zao la tumbaku na kuuza, mauzo ndani ya nchi na nje ya nchi, yote hayo yapo katika sheria ile nyingine.

Hii ya udhibiti wa bidhaa inahusika tu na bidhaa ambazo zimetengenezwa kiwandani na sasa zipo tayari kwa ajili ya kutumika, kwa mfano sigara, ndizo ambazo zimetajwa kwenye sheria ya bidhaa za tumbaku. Ila kweli ni ya muda mrefu na sasa inafanyiwa mapitio na Serikali ili iweze kuendana na wakati.

M24 TANZANIA:  Je, TMDA imewahi kupokea maombi ya usajili au uthibitisho wa bidhaa mbadala kama e-ciggarate?

TMDA: Tunapokea maombi, ndiyo kazi yetu, kwa mfano bidhaa za sigara tuna jumla ya maombi 41 hadi sasa, kwa sigara za kawaida. Kwa upande wa sigara za eciggarate na shisha bado sheria imekuwa kimya kwa bidhaa hizi kwamba zisimamiwe kwa utaratibu gani?. Ndiyo haya maeneo serikali imeelekeza kwamba sheria ya udhibiti wa tumbaku ifanyiwe mapitio kuweza kuweka vizuri utaratibu mzima wa kudhibiti bidhaa za shisha. 

Hizo e-ciggarate zote na ndiyo kinachofanyika sasa hivi, lakini bado Sheria ipo kimya na bidhaa hizo zipo nchini na zinaendelea kutumika. Hadi pale [ambapo] Sheria itakapokuwa imewekwa vizuri sasa kusema bidhaa kama hizo zisimamiwe namna gani?

M24 TANZANIA: Je mnaonaje dhana ya Tobacco Harm Reduction inayojadiliwa sasa hivi kimataifa, je ina nafasi yoyote katika udhibiti wa bidhaa za tumbaku nchini?

TMDA: [Of course] Sekta ya tumbaku na bidhaa za tumbaku nchini zinagusa wadau wengi sana na Wizara nyingi pia zinahusika kwenye biashara hizo zinatumika duniani kote, si tu Tanzania. Kweli ni bidhaa ambayo kiuchumi, inaongeza pato la taifa inaongeza fedha kwenye serikali nyingi, karibu zote [duniani] kikubwa ambacho kinafanyika sisi [kwa maana kama mamlaka za udhibiti] tunasema bidhaa za tumbaku, zinapaswa kuwa na viambata ambayo tunasema kitaalamu kwamba generally accepted not to cause harm.

Ndiyo misingi tunayoisimamia, kwamba viwango vyake vya nikotini, viwango vyake vya hatari viwe viwango ambavyo angalau vinakubalika kimataifa, visilete madhara kwa mtumiaji. Ndiyo kazi kubwa ambayo tunafanya hapa, na ndiyo maana nimetoka kusema zina kemikali 92 ambazo hizo ndizo harmful na ndizo ambazo hazitakiwi kuwa kwenye bidhaa za tumbaku.

Ndizo ambazo TMDA tunatakiwa kuhakikisha kila anayetengeneza bidhaa za tumbaku asitengeneze bidhaa ambazo ina hivyo viambata hai ambavyo vinaleta madhara makubwa kwa mtumiaji. Ni kazi tunayoifanya kila siku kuhakikisha [viambata hivyo] vinakuwa chini, vibaki vile viambata tu ambavyo tafiti ambazo zimefanyika angalau havina harmful effect sana kama ambavyo hizo 92 zipo kwenye bidhaa za tumbaku.

M24 TANZANIA: Changamoto gani ambazo mnakumbana nazo kuhusu bidhaa bandia na ambazo zinapitishwa kupitia njia za panya?

TMDA: Ni kweli nchi ina mipaka mirefu huwa tunakamata baadhi ya bidhaa za tumbaku ambazo ni bandia pia zinaharibu soko la bidhaa zetu za viwanda vya ndani. Tumekuwa tukichukua hatua mara kwa mara tunakamata na kuteketeza, tumeteketeza katika ofisi zetu za kanda mara kwa mara ili zisimfikie mtumiaji wa mwisho. Ni changamoto kubwa sana.

M24 TANZANIA: Je kwa mwaka 2023 au 2024 kulikuwa na matukio mangapi ya ukamataji wa bidhaa bandia za sigara ndani ya soko la Tanzania?

TMDA: Matukio yalikuwa kama manne [ya ukamataji bidhaa bandia zilizoingizwa sokoni kwa njia za magendo]. tumekuwa tukichukua hatua.

M24 TANZANIA:  Je, ni sigara mbadala ama sigara za kawaida ambazo zimezoeleka kwa wingi huko sokoni?

TMDA: Ni hizi sigara za kawaida.

M24 TANZANIA: Kwa sasa TMDA ina uwezo kiasi gani katika kupima bidhaa hizi mbadala?

TMDA:  Tuna maabara yetu pale Dodoma, tumeiweka mahususi kwa ajili ya upimaji wa bidhaa za tumbaku na dawa za mitishamba kutokana na 'nature' yake na kwa sasa tupo hatua ya kununua mashine za kisasa zaidi. Kwa sababu tumeshafanya utafiti kwa ajili ya kugundua/kujua mashine gani zinafaa kwa ajili ya kufanya upimaji/utafiti ambazo tutaziweka kwenye maabara yetu ya Dodoma ili kuweza kupima vizuri inavyopaswa bidhaa hizi za tumbaku.

M24 TANZANIA:  Ushirikiano na taasisi nyingine kwa mfano TBS [Shirika la Viwango Tanzania], Wizara ya Afya katika kudhibiti bidhaa hizi hasa katika kipindi hiki ambako nyingi zinaingia sokoni, upoje?

TMDA: Sheria inamtaja TBS kama ndiye mchunguzi mkuu ama analyst, yeye ndiyo ana wajibu mkubwa kufanya uchunguzi wa kimaabara wa bidhaa za tumbaku, sheria ndivyo inavyomtaka. TBS ni taasisi ambayo inaweka viwango, kwa hiyo hata sisi tukisema tunafuatilia tumbaku, kama ni kuangalia viwango ni lazima uhakikishe kwamba viwango vimepitishwa na TBS [ama national standars] kwenye masuala mazima ya bidhaa za tumbaku.

Tunashirikiana nao katika masuala hayo ya kiuchunguzi na kiudhibiti lakini pia suala la kuteketeza bidhaa tumbaku, dawa na bidhaa nyingine [tunazodhibiti] ni lazima tushirikishe watu wa NEMC [Baraza la Uhifadhi wa Mazingira].  Kwa hiyo masuala hayo wenzetu wa NEMC tunawashirikisha kuhakikisha uteketezaji unafanyika kwa mujibu wa utaratibu bila kuathiri mazingira na kuwa bila kuathiri afya za waliopo karibu wakati wa uteketezaji. Hivyo, wote tunashirikiana kwa ukaribu wakati wa uteketezaji.

M24 TANZANIA:  Vijana ni kundi linaloingia kwa kasi katika matumizi ya bidhaa mbadala zinazoingia sokoni ikiwamo eciggarate, shisha na nyinginezo. Je, mna mkakati gani wa kuwapa elimu ili wawe na uelewa kuhusu athari za matumizi ya bidhaa hizi mbadala.

TMDA:  Kwa sasa jukumu kubwa la kutoa elimu kwa Umma lipo kwa Wizara ya Afya, na sisi tujikite zaidi kwa ajili ya udhibiti. Kwa maana ya kutoa elimu kwa Umma, Wizara ya Afya imekuwa ikisimamia hilo eneo kwa kutoa semina mbalimbali, vipindi vya luninga na radio kuelimisha jamii ifahamu zaidi bidhaa hizi, utumiaji wake pia madhara yake na pia ikibidi kuweza, kupunguza watumiaji ili kulinda afya ya jamii.

M24 TANZANIA:  Kwa mtizamo wa TMDA je huu sasa ni wakati mwafaka kwa Tanzania kuwa na mjadala mpana pengine wa kitaifa juu ya bidhaa hizi mbadala na mnapendekeza hatua gani zichukuliwe, ikiwa tunaona kuna kasi ya utumiaji lakini Sheria bado ipo kimya?

TMDA: Niseme kikubwa kama kuhamasisha, kazi kubwa ya Wizara ya Afya ni kulinda afya ya jamii kwamba wananchi wabaki na afya njema, afya bora ili waendelee kuwa na nguvu na kuweza kusaidia katika ujenzi wa Taifa na kuleta tija kwenye nchi. Huu ni msimamo wa Wizara na sisi kama sehemu ya Wizara pia tunalisimamia ili kuhakikisha kwamba wananchi hawatumii bidhaa ambazo zinawaletea madhara, ndiyo sehemu kubwa ya kazi ambayo sisi kama sehemu ya Wizara kuhakikisha hilo linafanyika na linatendeka kumlinda mtumiaji wa mwisho.

M24 TANZANIA: Nilipata nafasi kuhakikisha mkutano wa Kimataifa wa TECHNOVATION 2025 ambapo uliangazia bidhaa mbadala za tumbaku, Tanzania je inajifunza nini kwa nchi ambazo zimesharuhusu bidhaa hizi mbadala na kuziwekea sera na miongozo ya usimamizi madhubuti?

TMDA:  Kwa sisi nchini mwetu, kwa mfano kupitia Sheria ya Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania hairuhusu matumizi ya bangi wala mirungi, kwa mfano ... ni kama bidhaa za tumbaku. aada ya kupima uzuri na mabaya wa matumizi haya bado inaonekana bidhaa hizi si nzuri kwa binadamu [hivyo] haziruhusiwi ndani ya nchi na ndivyo ilivyo, mtu yeyote haruhusiwi kulima, kutumia au kuuza bangi ndani ya nchi au kujihusisha na kitu chochote kinachohusisha bangi au mirungi na ndiyo msimamo wa nchi hadi sasa. 

M24 TANZANIA:  Je ni hivyo pia kwa bidhaa mbadala za tumbaku?

TMDA:  Hizo zote [bidhaa mbadala za tumbaku zenyewe] Sheria imekuwa kimya, bado haijasema hizi zitumike au zisitumike, kwa hiyo na sisi tunasimamia hapo hapo hadi pale mabadiliko ya Sheria yatakapofanyika na kuweka utaratibu kwamba inakuwaje kwenye bidhaa kama hizi.

M24 TANZANIA:  Je mpo tayari pia kuangalia nchi zingine zinafanyaje ili kujifunza namna zinavyofanya udhibiti wa bidhaa hizi?

TMDA:  Zipo nchi zinaruhusu nafahamu na zingine bado haziruhusu, kwa hiyo yote hayo wakati [huu] tunapitia Sheria, tutajua sasa, je hawa walioruhusu ni kwa sababu gani na hawa ambao hawajaruhusu ni kwa sababu gani, kwa hiyo tutajifunza huko ili kuona sasa na sisi tutakuwa na sheria gani nzuri ili kuhakikisha nchi inakuwa na utaratibu mzuri wa kusimamia bidha matatizo. 

M24 TANZANIA: Upi ujumbe wako wa mwisho kwa msomaji wa makala haya ambao unao ili umfikie au kwa waandishi wa habari hasa katika uelimishaji jamii kuhusu athari za matumizi ya bidhaa za tumbaku, nchini?

TMDA:  Tunajua waandishi wa habari ni vyombo vya muhimu kwenye nchi na ni wadau wa msingi kwenye nchi, ni kuendelea kuelimisha wananchi juu ya matumizi ya bidhaa hizi, mimi kama mtaalamu ambaye nimesoma masuala ya afya, sigara zina madhara, matatizo mengi kama saratani, shinikizo la damu yanasababishwa na matumizi ya bidhaa hizi, ndiyo maana hata ukisoma lebo za bidhaa hizi kuna maelezo yamewekwa yakitoa tahadhari, kwamba zinasababisha matatizo haya, ndiyo maana Wizara ya Afya imeweka udhibiti ili tuhakikishe tunalinda afya ya jamii.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement