Na Veronica Mrema - Tabora
Ufanisi wa utendaji kazi ndani ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba [TMDA] umeongezeka kwa kasi na viwango vya juu kufuatia hatua ya Serikali kuiongezea uwezo unaoendana na teknolojia za kisasa.
Hatua ambayo imeendelea kuipa nguvu zaidi TMDA katika kutekeleza majukumu yake ya kulinda afya ya jamii na kubwa zaidi usalama wa nchi.
Ndani ya kipindi cha miaka 4 tangu 2022 hadi 2025 TMDA imeshuhudia ikipiga hatua kubwa na kasi zaidi kiutendaji.
Dkt. Fimbo amebainisha, "Mojawapo ya mafanikio [ya TMDA katika miaka hii minne ni ongezeko la watumishi kutoka 261 hadi 439.
Amesema lengo lao lilikuwa kufikia watumishi 488 hata hivyo ingawa bado hawajaifikia kwa kiwango walichopokea hadi sasa ni zaidi ya 95% ya lengo lao la ajira mpya walizokusudia.
Hayo wameyapata katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Fimbo ameyabainisha, katika kikao kazi kati ya TMDA mamlaka iliyo chini ya Wizara ya Afya Tanzania pamoja na wahariri wa habari kutoka mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.
Kikao kazi hicho cha siku moja kimefanyika Mkoa Tabora ambapo ni ofisi kuu za TMDA kwa Kanda ya Magharibi.
Amebainisha kwa kina, “Kazi zetu kuu ni kusajili bidhaa, kufuatilia usalama wa bidhaa sokoni, na kufanya uchunguzi wa kimaabara.
"Yote haya yanawezekana kwa sababu sasa tuna nguvu kazi ya kutosha,” amesisitiza Mkurugenzi Mkuu huyo wa TMDA.
Amebainisha pia, ili kupanua wigo wa utendaji kazi wake Mamlaka hiyo imekamilisha ujenzi wa jengo la kisasa jijini Dodoma.
"Tuna na maabara mpya [ndani ya jengo hilo] imekamilika juni, mwaka huu jambo ambalo limeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi," amesema.
Ndani ya kipindi hicho pia TMDA imesimamia kuanzishwa kwa viwanda 18 vya dawa na vifaa tiba nchini vingi vikiwa mikoa ya Dar es Salaam, Kibaha na Arusha.
"Kila kiwanda kinawajumuisha wafanyakazi wapatao 170, [hatua hii] imechangia kutengeneza ajira mpya kwa wahitimu wa taaluma za afya na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Ameongeza "Katika usajili wa bidhaa, TMDA imesajili dawa zipatazo 8,332 na vifaa tiba 3,000.
"Hatua iliyosaidia upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa usalama na katika viwango vinavyokubalika kimataifa kwa ushirikiano na Wizara ya Afya na Wizara ya Viwanda na Uwekezaji.
Sambamba na hilo, TMDA pia mapato yake yameongezeka na wameweza kupeleka gawio la Tsh. Bil. 23 kwa Serikali.
Mamlaka hiyo, inaendesha uchunguzi kupitia maabara tatu za kisasa zilizopo Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza zote zikiwa zimeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani [WHO.
TMDA haijaacha nyuma suala la teknolojia kwani imeendelea kuimarisha mifumo yake ili kuendelea kuwafikia wateja kwa wakati mwafaka na kuondoa usumbufu katika suala la uombaji wa vibali.
"TMDA sasa inafanya shughuli zake zote kwa njia ya kielektroniki, ambapo mteja anaweza kuomba vibali na kuhudumiwa bila kufika ofisini.
"Hata akiwa nje ya nchi, maombi hupokelewa, kuchakatwa na kurudishwa ndani ya saa 24,” amesema Dkt. Fimbo.
Mfumo huo wa kielektroniki umesaidia ukaguzi wa mizigo bandarini na kwenye vituo vya forodha kwa kutumia wakaguzi walioko maeneo hayo, kurahisisha na kuharakisha utendaji kazi wa mamlaka hiyo.
Tangu mwaka 2021 TMDA imekuwa ikifanya kikao kazi na wahariri pamoja na waandishi wa habari ili kuongeza wigo wa uwasilishaji elimu kwa umma na taarifa juu ya utekelezaji wa majukumu yake.
"Ushirikiano na vyombo vya habari umekuwa nguzo muhimu ya mafanikio yetu," amesisitiza na kuongeza,
"Tunatambua mchango mkubwa wa wahariri na waandishi wa habari katika kufanikisha malengo yetu.
"Kwa kutambua hilo, tuna utaratibu wa kutoa tuzo kila mwaka [tangu kikao hicho cha kwanza ambapo walipitisha azimio la pamoja] waandishi wanaofanya kazi nzuri tunawapa tuzo,” ameweka wazi.
Amedokeza zaidi, "Mamlaka hii haiwezi kufanya kazi zake kwa ufanisi bila ushirikiano wa karibu na wadau wa habari ambao ni kiungo muhimu kati ya TMDA na wananchi.
“Kupitia waandishi na wahariri, jamii inaweza kufikiwa haraka na kwa ufanisi kuhusu matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba,”.
Awali, Mhariri wa habari Clouds Media Group ambaye aliteuliwa kuongoza kikao kazi hicho kwa nafasi ya Mwenyekiti, Joyce Shebe akizungumza amesema kalamu za wanahabari zina uwezo mkubwa.
".., wa kufikisha ujumbe mbali na kwa haraka, hivyo ni wajibu wetu kushiriki kikamilifu katika kuipa jamii taarifa hizi, hivyo ni vizuri kuelimishwa kwanza sisi ili twende kuelimisha vizuri zaidi," amesema.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Honoratha Rutanisibwa akimwakilisha Afisa Tawala Msaidizi wa Mkoa [RAS] ameshiriki kikao kazi hicho.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa huo kukifungua rasmi, amesema "TMDA katika Kanda hiyo imekuwa ikishirikiana vema na Ofisi ya Mkoa na halmashauri.
"Tunaposhirikiana na TMDA katika ukaguzi na utoaji wa elimu, tunaongeza ufanisi katika kudhibiti dawa zisizo na ubora. Hii ni njia bora ya kuwalinda wananchi dhidi ya madhara ya dawa zisizo salama.
"Nampongeza mno Meneja wa Kanda hii ya Magharibi, ana ushirikiano mzuri nasi na tunafikia jamii kuisaidia pia wamekuwa wakikagua vifaa tiba na vitendanishi ndani ya hospitali zetu," amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha akifungua kikao hicho amepongeza hatua ya TMDA kufanya kazi bega kwa bega na wahariri pamoja na waandishi wa habari.
“Usimamizi mzuri wa bidhaa za afya ni msingi wa kuhakikisha afya za wananchi zinalindwa," amesema na kuongeza,
".., tunathamini sana ushirikiano huu kati ya TMDA na vyombo vya habari ili kuhakikisha ujumbe wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi unafika kwa watu wengi kwa usahihi na kwa wakati,".
Kikao hicho ni sehemu ya mikakati ya TMDA ya kuendelea kuelimisha umma kuhusu kazi zake, sheria zinazotumika na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia.
Lengo madhubuti ikiwa ni kujenga jamii yenye uelewa wa kutosha kuhusu matumizi salama ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini.
Chapisha Maoni