moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

Kila siku kunazaliwa zana, kurasa na majukwaa mapya ya kidigiti yenye uwezo mkubwa katika uundaji wa maudhui ya aina mbalimbali kwa haraka na urahisi zaidi. 

Akili Unde (AI) ni teknolojia ambayo imeendelea kukua na kuenea kwa kasi ya ajabu duniani. 

Tafsiri yake inaweza kusemwa, dunia iko katika kilele cha mapinduzi ya kidigitali na kila uchao kuna mabadiliko mapya yanayochochewa na teknolojia hii ya AI.

Miaka ya hivi karibuni, teknolojia ya AI imechochea dhahiri kasi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo mawasiliano na kurahisisha upatikanaji wa taarifa kupitia mitandao ya kijamii.

Katika muktadha huu, Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2025 utakuwa wa kipekee katika historia ya nchi.

Si tu kwa sababu ya ushindani wa kisiasa, bali pia kwa kuwa ni uchaguzi wa kwanza kufanyika katika kipindi ambacho AI imepiga hatua kubwa duniani.

Kwa Taifa la Tanzania lililopo Ukanda wa Afrika Mashariki, haya ni muda nyeti na umakini unpaswa kuongezwa hasa kwa suala la usambazaji wa maudhui.

Uandishi wa habari katika zama hizi za teknolojia ya AI unahitaji weledi wa hali ya juu, ufuataji wa maadili na kufanya uchambuzi wa kina wa taarifa kabla ya kuziripoti. 

Uchaguzi Mkuu wa 2025 utakuwa kipimo kikubwa cha jinsi waandishi wa habari watakavyoweza kutumia teknolojia kwa faida ya Taifa bila kuwa chanzo cha migogoro

Teknolojia hii inafanya taarifa kusambaa kwa sekunde chache tu, ndiyo maana ni muhimu kuongeza umakini wa hali ya juu, hasa kwa waandishi wa habari, vyombo vya habari na hata wapiga kura.

AI inaweza kuwa na manufaa makubwa endapo itatumika kwa uangalifu lakini bila udhibiti sahihi, inaweza vile vile  kusababisha madhara ikiwamo usambazaji wa taarifa potofu [misinformation], propaganda na uchochezi. 

Hali hii inahitaji uandishi wa habari makini ambao unazingatia weledi, maadili na utafiti wa kina, pamoja na kulinda utu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania [TAMWA], Silvia Daulinge anasema nyakati hizi kila mwandishi wa habari anapaswa kuwa makini.

"Ni muhimu, waandishi wa habari  kuwa makini sana na matumizi ya AI ili kuhakikisha wanakuwa salama na wanatunza amani katika Uchaguzi Mkuu," anasema.

TAMWA kwa kushirikiana na taasisi ya GIZ ya Ujerumani, waliandaa mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini.

Lengo kuu ni kuwawezesha waandishi wa habari kuwa na uelewa mpana kuhusu matumizi ya AI na namna ya kujikinga na taarifa tatanishi hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi.

Kwa nyakati tofauti baadhi ya waandishi walionufaika na mafunzo hayo maalum, wameeleza kile walichojifunza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025.

"Tumehimizwa kuwa makini zaidi hasa katika kipindi hiki cha matumizi ya Ai, kabla ya kusambaza taarifa ambazo tunakuwa tunazipokea, au kuziona mitandaoni," anasema Timothy Marko

Anaongeza "Mada ya Ai kuelekea Uchaguzi Mkuu imevunitia zaidi kwa kuwa ni eneo linalokua kwa kasi na linaathiri kazi ya habari.

"Matumizi ya AI ni makubwa, ni muhimu kwetu waandishi wa habari kuwa makini sana katika kuchambua habari zetu kabla ya kuzisambaza," anasema.

Daulinge anasisitiza waandishi wa habari wanapaswa kufanya uchambuzi wa kina wa taarifa kabla ya kuziripoti au kuzisambaza.

Tafiti zinaonesha taarifa tatanishi zimekuwa chanzo cha vurugu za kisiasa katika sehemu mbalimbali duniani, kwa mujibu wa Daulinge.

"[Hivyo] ni vyema waandishi wa habari nchini wakazingatia maadili ya taaluma yao na kuepuka kuripoti habari zenye mlengo wa kuchochea migawanyiko katika jamii," anasema. 

Aurelia Semtoe wa Mwananchi anasema yamemsaidia kumuongeza uelewa wake kuhusu wajibu binafsi anaopaswa kufanya kama mwandishi wa habari.

"Hasa wa kutokusambaza au kushiriki kwa namna yoyote katika kusambaza taarifa zenye kuchochea chuki dhidi ya mtu au kundi lolote.

"Nimeongezewa ujuzi zaidi katika kuangazia kwa kina na kuhakikisha sitakuwa sehemu ya hate speech dhidi ya wengine, mtandaoni," anasema Aurelia.

Kwa upande wake, Avila Kakingo wa Michuzi Blog anasema amejifunza kuepuka kauli au maandiko yanayobeba upotoshaji, ambao huweza kuathiri jamii kwa mtazamo hasi na kuchochea mgawanyiko.

Mkuu wa Programu ya Amani kupitia mpango wa Global Action for Peace Building [Defyhatenow] Njoki Karuki anasema waandishi wa habari wanapaswa kujiepusha na taarifa zinazotweza utu wa mtu au kuleta chuki na mgawanyiko.

"Ni muhimu kufanya uchambuzi wa kina wa vyanzo vya habari nani amesema, amesema lini, amesema wapi, na kwa nini amesema hivyo," anasema Njoki.

Anasema badala ya kusambaza taarifa za uchochezi, waandishi wa habari wanapaswa kusikiliza sera za wagombea na kuripoti kwa uadilifu.

"Tusisikilize maneno ya mitandaoni yasiyo na uthibitisho. Tusambaze taarifa zinazojenga umoja, si chuki na mgawanyiko," anasema Njoki.

Anaongeza "Hata kitu / ujumbe gani 'una-comment' kwenye mtandao unapaswa kuwa makini pia, kwa sababu inaweza kuleta madhara.

Winfrida Nyagawa anasema mafunzo hayo yamekuwa yenye manufaa makubwa kwao kwa kuwapa nafasi ya kupanua maarifa yao.

"Tumekumbushwa kabla ya kuripoti au kusambaza taarifa fulani, tujiulize maswali kadhaa kwa mfano, mzungumzaji alikuwa nani? Alikuwa wapi?.

"Je, alikuwa anaongea na nani? na alikuwa katika hali gani? ili kuepuka kusambaza 'misinformation' na malinformation," anaeleza.

Florence Majani kutoka TAMWA anasema katika zama hizi za kidigitali kundi la wanawake limekuwa likiathirika kwa kiwango kikubwa kwenye majukwaa ya mitandaoni.

"Ukitazama tu ndani ya jamii, mwanamke amekuwa akikabikiana na dhana nyingi potofu, kuna vyakula baadhi ya maeneo mwanamke haruhusiwi kula.

"Mwanamke akiingia kwenye siasa napo kuna changamoto, mitandaoni tunaona namna baadhi ya wanavyokabiliwa na ukatili," anasema.

Anasema wapo baadhi ya wanasiasa wanawake ambao wamesitisha kabisa kutumia majukwaa ya mitandaoni ili kuepuka ukatili.

"Kipindi hiki cha AI unaweza kukutana na taarifa ya kutengeneza, ambazo hata hazina uhalisia, dhidi ya mgombea fulani. Umakini unahitajika.

Raymond Nyamwihula wa Azam Media anasisitiza kwamba mafunzo hayo yamewapa ukumbusho kwa wanahabari kuhusu msingi wa taaluma yao kusaka ukweli zaidi.

"Juu ya jambo fulani ni muhimu ili kujihakikishia kile unachokwenda kukiwasilisha kwa jamii ni sahihi," anasema Raymond.

Naye Kijoli Chikopa wa Wapo Media anaongeza "Waandishi wa habari wanapaswa kuwa na weledi katika kazi zao na kufuata maadili ya taaluma.

"Tuepuke kusambaza misinformation, darasa hili limetukumbusha tufanye kazi kwa kufuata maadili ya taaluma ya habari, ili tusiwe chanzo cha kuleta mikanganyiko ndani ya jamii,".

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement