moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Kila daktari mmoja aliyefadhiliwa masomo yake kupitia Merck Foundation, anahudumia zaidi ya wagonjwa 1,000 ndani ya Taifa lake, Barani Afrika.

Miongoni mwao kuna ambao wanatoa huduma katika hospitali za Umma na wengine katika maeneo ya pembezoni [vijijini] ambako awali huduma hizo zilikuwa hazipatikani kabisa.

Merck Foundation inataja takwimu hiyo ni matokeo chanya katika moja ya program zake ambazo lengo lake ni kuhakikisha jamii inafikiwa kwa huduma hizo muhimu.

Mtendaji Mkuu wa wakfu huo Seneta Dkt. Rasha Kelej katika mkutano wa 7 wa MFFLI uliofanyika Dubai, mwaka huu 2025, anasema jumla ya madaktari 2,270 kutoka nchi 52 wamepata ufadhili.

"Ni kwa fani muhimu 44 za tiba ambazo katika mataifa yao hakukuwahi kuwapo wataalamu wa fani hizo, hapo kabla ya ufadhili wa mafunzo kupitia Merck Foundation," anasema.

Kwa hatua hiyo, Merck Foundation inasema sekta ya Afya na elimu kwa agenda mahususi ya kumuinua mwanamke na mtoto wa kike chini ya MFFLI inaendelea kufanya mapinduzi makubwa.

Kwa kasi inayovutia na kuridhisha, MFFLI ni Mpango wa Merck Foundation First Ladies Initiative ambapo wakfu huo unashirikisha moja kwa moja wake wa marais, ambao ni mabalozi wake wakuu.

First Ladies hao ni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, takwimu za Merck Foundation zinaonesha maelfu ya maisha yanabadilishwa kupitia mpango wa elimu kwa madaktari pia kuwezesha wasichana.

Dkt. Rasha anaongeza "Kwa mara ya kwanza, nchi nyingi sasa zina madaktari bingwa katika magonjwa kama saratani, kisukari, afya ya akili, uzazi, magonjwa ya watoto na huduma za dharura."

Anasisitiza udhamini huo umeleta mapinduzi ya kweli katika upatikanaji wa huduma za afya bora.

JAMII ZAIDI

Oluremi Tinubu ni Mke wa Rais wa Nigeria anasema mpango huo wa Merck Foundation ni wa kupongeza kwani unainufaisha jamii moja kwa moja.

Anasema atapanua zaidi mpango huo nchini kwake kupitia ofisi yake na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

"Nakubaliana kabisa kuwa huu ni mpango wenye manufaa makubwa kwa nchi yetu,".

Anaongeza "Nitajitahidi kuuendeleza zaidi kupitia ofisi yangu. Hii itawawezesha madaktari wa Nigeria kutoa huduma bora kwa wananchi wetu.

Anasema ni mpango mzuri kuwapa mafunzo wataalamu wa afya hatua ambayo inaimarisha huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi ambako kwa nchi nyingi ndiko kuna idadi kubwa ya watu

Anasema kuwawezesha wasichana kupitia elimu ni msingi wa kujenga jamii zenye afya na usawa.

"Kupitia mpango wa Renewed Hope Initiative [aliouanzisha] wanaendelea kutekeleza miradi ya kuwawezesha vijana, hasa wasichana, kupata elimu na kujikomboa kiuchumi,"

EDUCATION LINDA

Ni program ambayo Merck Foundation imejikita kusaidia kuendeleza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na ukosefu wa elimu kwa wasichana.

Kwa mpango huo hutoa udhamini wa elimu kwa zaidi ya wasichana 1,000 katika nchi 17 kupitia mpango wa Educating Linda.

"Kuwawezesha wasichana kupata elimu ni zaidi ya msaada wa kifedha ni uwekezaji katika mustakabali wa taifa zima.

"Tunapambana dhidi ya ndoa za utotoni na ukatishaji wa ndoto zao,” anasema Seneta Dkt. Rasha na kusisitiza,

"Wasichana hao hupatiwa msaada wa ada, sare, vifaa vya shule na ufuatiliaji wa maendeleo yao hadi kumaliza shule, kwa kushirikiana na wake wa marais wa mataifa husika."

Mke wa Rais wa Kenya Rachel Ruto anasema nchi hiyo pia imenufaika kwa uwepo wa jukwaa hilo la MFFLI la Merck Foundation.

Anasema wanayo dhamira ya kuendelea kuimarisha sekta ya afya na elimu hasa kwa mtoto wa kike, kupitia ushirikiano wa muda mrefu na Merck Foundation.

Nchi hiyo iliyopo Ukanda wa Afrika Mashariki imenufaika kupata ufadhili wa madaktari 244 kwa mafunzo ya ubobezi katika fani 44 za tiba.

Anabainisha 50% ni wanawake jambo ambalo linachangia kuwawezesha wanawake katika taaluma ya afya.

"Kwa mpango wa “Educating Linda”, wasichana 47 kutoka familia zisizojiweza nchini Kenya wanaendelea kufadhiliwa kutoka sekondari hadi chuo kikuu," anabainisha.

Anaongeza "Kenya pia inaandaa kundi la wanafunzi 100 kusomea stashahada ya juu ya 'Clinical Nutrition' katika Chuo Kikuu cha Buckingham, Uingereza kupitia Merck Foundation.

"Merck Foundation si tu inafadhili elimu, bali inabadilisha maisha ya familia na jamii kwa ujumla.

"Kila msichana nchini Kenya na Afrika kwa ujumla anastahili nafasi ya kutimiza ndoto zake iwe ni kuwa daktari, mhandisi, mwalimu au mwanasayansi," anasema na kusisitiza,

"Tunaendelea kusomesha madaktari si kwa ajili ya Wakenya tu, bali pia kwa ajili ya ndugu zetu Waafrika wanaotafuta tiba nchini mwetu."

"Tunaamini furaha ya maisha inatokana na kumsaidia mtu mwingine na hii ndiyo kazi kuu ya Merck Foundation," anasema.

TUZO / UHAMASISHAJI

Sekta ya habari, sanaa ni eneo ambalo Merck Foundation haijaliacha nyuma, amesema majukwaa hayo wamekuwa wakiandaa tuzo maalum ili kuhamasisha uwasilishaji bora kwa agenda wanazozisimamia.

Dkt. Rasha anasisitiza vyombo vya habari na sanaa vina mchango mkubwa katika kusaidia kubadilisha mitazamo ya jamii.

".., kuhusu afya, ndoa za utotoni na unyanyapaa unaotokana na hali kama utasa au magonjwa ya muda mrefu," anasema.

Anaongeza “Waandishi wa habari wa afya, wanamuziki na watayarishaji wa filamu tunawachukulia kama mashujaa wa mabadiliko.

"Kupitiao wao tunaingia kila nyumba kwa njia ya sauti na picha tukibeba ujumbe wa matumaini, elimu na mabadiliko ya kitamaduni,” amesema.

Mamilioni ya watu wameweza kufikiwa na Merck Foundation kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii, redio na runinga, mashindano ya ubunifu na warsha za kitaaluma.

Mkutano huo umefuatwa moja kwa moja na zaidi ya watu milioni 8 mtandaoni, na wengine 6,000 ambao walihudhuria kwa njia ya mtandao.

Mke wa Rais wa Ghana Lordina Dramani Mahama anasema Merck Foundation imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya nchini Ghana na bara la Afrika kwa ujumla.

Anabainisha vijana 110 kutoka Ghana wamenufaika na programu za Merck Foundation ikiwamo katika sekta ya muziki/sanaa.

"Teknolojia ya habari na mawasiliano [ICT], utengenezaji wa filamu, na mitindo ya mavazi [fashion], na kuwajengea imani na mwelekeo wa maisha.

"Nina dhamira ya dhati kuendelea kuimarisha ushirikiano wa Merck Foundation na Lordina Foundation [taasisi ninayoiongoza]," anasisitiza.

Anasema lengo ni kuendeleza upatikanaji wa huduma za afya na elimu kwa jamii huku akitoa wito wa mshikamao katika kutetea haki na ustawi wa wanawake na watoto Barani Afrika.

MFFLI PAMOJA

Mke wa Rais wa Maldives, Sajidha Mohamed, anahimiza kuimarishwa kwa ushirikiano zaidi ili jamii wanazozihudumia ziendelee kupata manufaa kwa mpango huo wa Merck Foundation.

Anabainisha nchini mwao, "Bado kuna uhaba mkubwa wa wataalamu katika fani maalum kama tiba ya uzazi na embryology.

Anaishukuru Merck Foundation kwa kutoa udhamini wa mafunzo kwa madaktari wa Maldives katika maeneo hayo nyeti.

Anasema wanaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora na nafuu za afya katika visiwa vyote vya nchi hiyo.

Maeneo yao ya kipaumbele ni pamoja na uchunguzi wa saratani, afya ya akili, na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi wa sekta ya afya.

Merck Foundation pia inafanya vizuri katika kampeni zake za kupinga unyanyapaa dhidi ya waliokosa watoto, ukatili wa kijinsi na kuchagiza mtindo bora wa maisha kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.

"Ni kampeni zenye tija kwa jamii," amesema na kuongeza "Tunao Mpango wa Usawa wa Kijinsia wa Maldives.

"Unaweka mikakati ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wanawake, na kuzuia ukatili dhidi yao.

DIRA ENDELEVU

Tanzania haipo nyuma katika agenda hii, inao madaktari ambao wamesoma kwa ufadhili wa Merck Foundation ngazi ya ubingwa kwa fani mbalimbali muhimu za tiba.

Ikiwemo afya ya uzazi, tiba ya saratani, tiba ya akili, upasuaji, na magonjwa sugu. Hii imesaidia kuongeza idadi ya wataalamu bingwa nchini.

Ndani ya hospitali za umma ambako huduma hizo awali zilikuwa hafifu au hazipo kabisa.

Kampeni za uhamasishaji juu ya afya ya uzazi, unyanyapaa wa ukosefu wa uwezo wa kupata mimba, na magonjwa yasiyoambukiza zimekuwa zikifanyika kwa nguvu.

Hasa kupitia vyombo vya habari na waandishi wa habari ambao hupata mafunzo ya Merck Foundation kwa ushirikiano na madaktari ambao pia ni mabalozi wake. 

Dira ya Merck Foundation ni mabadiliko endelevu, kwa mujibu wa Dkt. Rasha, wataendelea kufadhili kila mwaka madaktari na wasichana.

Vile vile, wataendelea kushirikiana na wake wa marais katika kuimarisha afya ya uzazi, kutokomeza unyanyapaa wa utasa, na kupaza sauti dhidi ya ndoa za utotoni.

"Hili si jambo la mwaka mmoja, bali ni safari ya pamoja ya kubadilisha mustakabali wa afya na elimu Afrika. 

"Tuna nia thabiti, kuendeleza kasi hii hadi kila mtoto na kila mgonjwa apate huduma anayostahili," anasema.

MFFLI inathibitisha mabadiliko Barani Afrika yanawezekana yakiongozwa na ushirikiano thabiti pia uwekezaji kwenye elimu na afya, na dhamira ya kweli ya kuwainua walio pembezoni.

Mkutano huo ulihudhuria na wake wa marais kutoka Kenya, Angola, Nigeria, Zimbabwe, Maldiives, Ghana na kwengeko.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement