moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema 

Ni mtaalamu mbobezi na nguli zaidi katika masuala ya afya ya moyo, mtafiti mahiri, kiongozi makini mwenye sifa lukuki ndani na nje ya nchi.

Profesa Mohamed Yakub Janabi wengi wetu nchini Tanzania tunafahamu utendaji kazi wake ulioacha alama njema katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete [JKCI] alipokuwa Mkurugenzi Mtendaji.

Hivi sasa ni Mkurugenzi Mtendaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili [MNH] pia ni Mshauri wa Rais wa Tanzania katika masuala ya afya.

Aidha, ndiye mtaalamu pendekezwa ambaye anatarajiwa kwenda kugombea Ukurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika [WHO-AFRO].
Ukipata bahati ya kufanya naye kazi kwa ukaribu zaidi au kuhudumiwa naye au kufuatilia nyendo zake katika utendaji kazi wake, atabaini uongozi ni kipawa alichojaliwa na Mwenyezi Mungu. 

Ni mtu wa watu, anayependa matokeo chanya na ustawi bora wa afya ya mtu mmoja mmoja, familia, Taifa, Afrika na bila shaka dunia kwa ujumla. 

Jina lake ni gumzo kila kona, siri kubwa iliyo nyuma ya mafanikio ni ushupavu, usikivu na ule uchapakazi wake. 

Ufanisi wa kipekee pia katika kuihudumia jamii kupitia taaluma yake ya udaktari anayoipenda mno kutoka katika kilindi cha moyo wake. 
Prof. Janabi amebeba tumaini kwa mara nyingine kuipeperusha bendera ya Tanzania katika anga la Bara la Afrika kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuwania tena nafasi ya Ukurugenzi Mkuu wa WHO-AFRO. 

Nafasi hii ipo wazi kufuatia kifo cha Dkt. Faustine Ndugulile kilichotokea Nov. 27, 2024, nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu. 

Dkt. Ndugulile ingawa hakujaliwa kukalia kiti hicho lakini ameiwekea heshima kubwa Tanzania ya kuwa Mtanzania wa kwanza na mwana-Afrika Mashariki wa kwanza kushinda nafasi hiyo. 

Enzi za uhai wake pia alifanya kazi nzuri akiitumikia Tanzania katika nafasi ya Unaibu Waziri wa Afya. 

Ameacha alama bora kwa wananchi aliowatumikia huko Kigamboni akiwa ndiye Mbunge wao wa pekee aliyeongoza kwa mihula mitatu mfululizo. 

Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahala pema peponi kwani hakika ameandika historia njema itakayokumbukwa vizazi na vizazi. 
“Tutagombea tena nafasi ile ya WHO-AFRO,” kauli yake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa katika Misa ya kuuaga mwili wa Dkt. Ndugulile. 

Rais Samia akategua kitendawili cha nani ambaye atakwenda kuipambania tena nafasi hiyo na hapo likatajwa jina la Prof. Janabi. 

"Nimekuteua kuwa Mshauri wa Rais Mambo ya Afya lakini bado nataka 'utupe jicho' Muhimbili, lakini jingine ninatoa siri hapa hapa.

"Tumeangalia CV kama tano za wenzio, tukaona yako tunaweza kuipeleka kwenye 'competition' ile ya WHO,".

"Kwa hiyo tunakutayarisha kwenda huko wakati ukifika tutapeleka CV yako na tutakuingiza kwenye kushindania nafasi hiyo kuanzia sasa jiandae kwa hilo, pamoja na ushauri wa Rais, tutakupeleka huko".

Ni kauli ya msisitizo kutoka kwa Rais Dkt. Samia aliyoitoa ndani ya Ikulu ndogo ya Tunguu, Visiwani Zanzibar, alipowaapisha viongozi wapya ambao aliwateuwa hivi karibuni. 

Nikukaribishe sasa tuiangazie safari ya Prof. Janabi hatua zake na alama za kipekee ambazo zinampa thamani zaidi katika kuelekea kinyang’anyiro hicho. 
'USHAWISHI' 

Ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa ndani ya jamii ya wanataaluma wenzake, wanasiasa na jamii ndani na nje ya Tanzania. 

Unaweza kumpa ‘taswira’ ya ‘mchonga njia’ kwa aina yake ya uongozi wenye ushawishi kiasi cha kupaisha kasi ya utendaji kazi katika nafasi anazopewa kuzisimamia. 

Prof. Janabi si kiongozi anayependa kukaa tu ofisini kwenye kiti chake ni mtu wa kazi, utamkuta huku na kule akisimamia utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. 

Nikurudishe nyuma kidogo mnamo mwaka 2013/14 alipokabidhiwa 'kijiti', kuongoza kilichokuwa Kitengo cha Tiba ya Moyo ndani ya Hospitali ya Taifa Muhimbili [MNH]. 

Mtangulizi wake Dkt. Robert Mvungi alianzisha mwendo na Prof. Janabi akauendeleza kwa kasi zaidi na ubunifu zaidi. 

Binafsi niliziona juhudi zake, tangu akiwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji na baadae akawa Mkurugenzi Mtendaji kamili baada ya kuanza rasmi kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete [JKCI]. 

Septemba 5, 2015 ilipoanza hadi kufikia 2022 alipohamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili [MNH] mengi aliyoyatenda JKCI ni alama zisizofutika. 

Alipoipokea JKCI kulikuwa na wagonjwa kati ya 200 hadi 350 kwa mujibu wa ripoti za Wizara ya Afya ambao walikuwa wakipelekwa nje ya nchi kwa matibabu. 

Idadi hiyo ni ya watu wanaokabiliwa na magonjwa mbalimbali hususan yasiyoambukiza [NCDs] ikiwamo figo, saratani na wengi zaidi ya hao walikuwa ni wa moyo. 

Idadi hiyo ni sawa na 95% ya wagonjwa waliokuwa wakienda nje kila mwaka kwa matibabu, na kila mmoja wao aliigharimu Tanzania kiasi cha Tsh. Mil. 30 kwa matibabu. 

Sikuona tena jambo la ajabu kumkuta Prof. Janabi mstari wa mbele akiongoza watumishi wake katika utekelezaji wa majukumu yao pia. 

Misingi mizuri na imara ikiwamo uwekezaji wa mashine za kisasa JKCI, MNH, MOI, Ocean Road na taasisi nyingine zimeipaisha Tanzania. 
MAONO MAKUBWA 

Siku zote ni mtu mwenye maono makubwa, siku moja alisema ‘nataka JKCI iwe Apollo ya Afrika’. 

Nikaandika makala na kuyachapa Des. 14, 2017 yakiwa na kichwa cha habari ‘JKCI na ndoto ya kufikia viwango vya Apollo, ndani ya Blog hii. 

April 7, 2022 nikaandika na kuchapa makala nyingine sasa haikuwa ndoto tena bali ni halisi ikiwa na kichwa cha habari ‘Apollo ya Afrika’: Si ndoto tena Tanzania viwango kimataifa tiba ya moyo. 

Makala hayo yanaeleza kwa kina mengi yaliyofanyika hadi kufikia hatua hiyo DRC Kongo ilikuwa nchi ya kwanza kuanza kuleta watoto wake wanaohitaji matibabu miaka mingi iliyopita. 

Ikafuatiwa na wengineo ikiwamo Malawi, Comoro, Zambia na nyinginezo nyingi sasa si tu wagonjwa bali hadi wataalamu wake wanakuja kupata mafunzo ndani ya JKCI. 

‘Tumebakiza hatua chache kupandikiza moyo, kuna siku tutafika huko,” aliniambia JKCI sasa ipo hatua nzuri zaidi ikitumia teknolojia za kisasa na misingi imara ya mshikamano aliyoijenga.
JUHUDI 'HUZAA MATUNDA' 

Mabalozi hawakuisha kupishana kuingia na kutoka, kambi za ubingwa na ubobezi zikafanyika kila mwaka, wataalamu manguli walitoka katika nchi zao wakatua Tanzania ndani ya JKCI. 

Haikuwa ajabu tena kumuona Prof. Janabi akishiriki baadhi ya kambi hizo ni kiongozi wa mfano wa aina yake.

Haikuwa ajabu tena kumuona, maeneo walipoketi ndugu wa wagonjwa wakisubiri huduma, akizungumza nao, akiwauliza kuhusu huduma iwapo wanaridhika nazo au la.

Haikuwa ajabu tena pia kumuona wakati mwingine akiwapa elimu kujikinga na NCDs. JKCI ikazidi kusonga mbele.

Tukaanzisha Jarida la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete pamoja na akaunti ya Youtube kupeperusha zaidi habari pamoja na kuimarisha ushirikiano na vyombo vingine vya habari.

Miaka ilivyosonga mbele, elimu ya afya ya moyo ikaongezeka zaidi na zaidi kwa jamii, ni hatua muhimu tuliyoifurahia. 

Alihakikisha kila kada inatimiza wajibu wake kuanzia mlinzi, mtu wa usafi, wauguzi, madaktari na nyingine zote. 

Ule msemo wa umoja ni nguvu utengano ni udhaifu tunaona mantiki yake, ndani ya muda mfupi sana, Taasisi nzima ikawa kitu kimoja na huduma zikawa imara zaidi.
MAISHA KWANZA 

Ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa katika kujenga hoja na kuitetea ikaonekana tija yake kwa upana zaidi. 

Uwekezaji mkubwa ukashuhudiwa wa vifaa tiba vya kisasa vya mabilioni ya fedha ndani ya JKCI uliofanywa kwa sehemu kubwa na Serikali ya Tanzania. 

Ndani ya miaka michache tu matokeo chanya yakaanza kuonekana kwa kasi kubwa.

Magonjwa ya moyo yalikuwa ni kati ya yale yaliyochangia idadi kubwa ya watu waliosafirishwa kwenda nje ya nchi kufuata huduma mambo yakageuka.

Idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi ikiwamo hao wa moyo ikaanza kupungua kadri siku zilivyosonga mbele na leo hii 95% ya wagonjwa hao wanatibiwa ndani ya nchi. 

"Furaha yetu kubwa ni kuona namna tunavyookoa maisha ya watu zaidi licha ya ukweli kwamba pia tunaokoa fedha za Serikali ambazo zingetumika kuwatibu nje ya nchi,”.

Ni kauli ambayo Prof. Janabi huisema mara nyingi akiwa katika mikutano yake na waandishi wa habari hata sasa. 

KIMBILIO LA AFRIKA

Ule utendaji bora wa JKCI umeendelea kuwa mvuto wa aina yake ya kwa mataifa mengine ya Afrika, mabalozi wa nchi mbalimbali wanazidi kuingia makubaliano na Tanzania kuleta wagonjwa wake.

Haikuwa safari nyepesi kufikia hatua hizo ilihitaji usimamizi madhubuti hasa kujenga ule msingi wa MSHIKAMANO na hili alifanikiwa kwa zaidi ya 100%. 

Kipindi cha janga la UVIKO – 19 kilikuwa kigumu kwa kila nchi kwani ilikuwa ikipambana kwa namna yake kusaidia raia yake dhidi ya janga hilo.

Prof. Janabi bado alisimama tena mstari wa mbele kutoa elimu kwa jamii kuhusu janga hilo na hata chanjo ya UVIKO – 19, alizichambua na kuzifafanua vema.

Imani huzaa imani, mwaka 2022 akateuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili akaaicha JKCI katika mikono salama ya vijana wake, Dkt. Peter Kisenge akateuliwa kuiongoza JKCI.

Akiiongoza Muhimbili Prof. Janabi ni yule yule wa JKCI hajapoa kwa kiwango kikubwa pia amefanikiwa kuzikonga nyoyo za Watanzania.

Mstari wa mbele bado yupo, ameipendezesha Muhimbili sasa ina sura ya hospitali ya Taifa, amefanya kazi kubwa pia kuimarisha mahusiano ya wafanyakazi wake.

Somo la huduma bora kwa mteja likaendeshwa kwa wafanyakazi ili kuhakikisha jamii inahudumiwa vema.

Kwa kiasi kikubwa amefanikiwa kujenga imani kwa jamii, somo la kuepuka NCDs ndilo linalovuma kwa kasi ndani ya jamii.

Akaona haitoshi akaandika kitabu cha Mtindo Bora wa Maisha, tuzo kedekede akajizolea ikiwamo ile ya Mshua Master.
UTALII TIBA 

Hili ni zao jipya ndani ya sekta ya afya Tanzania, Prof. Janabi anasema Afrika hupoteza fedha nyingi kupeleka wagonjwa nje ya nchi kufuata matibabu.

Fedha hizo zinaweza kuokolewa kwa kuimarisha na kuboresha huduma za tiba ndani ya mataifa ya Afrika.

Ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa inayoshughulikia Utalii Tiba, ameweka msingi mzuri na sasa Tanzania imeanza kuona matunda yake.

Ndani ya Muhimbili amesimamia uanzishwaji wa huduma za ubobezi zaidi ya 13 ikiwamo upandikizaji uloto, upandikizaji figo kwa njia ya matundu, upandikizaji nyonga na magoti.

Upandikizaji puto kwa wanaokabiliwa na unene na uzito ulipitiliza, tiba ya ngozi, urekebishaji mwili [Plastic Surgery], upandikizaji mimba.

Uvunjaji mawe kwenye figo kwa kutumia mawimbi mtetemo, uondoaji uvimbe kwenye ubongo kwenye sakafu ya ubongo kwa kupitia matundu ya pua na nyinginezo.

Kwa kuanzishwa huduma hizo Tanzania imeendelea kushuhudia ongezeko la wagonjwa kutoka nje ya nchi pia ambao wanakuja ili kutibiwa Muhimbili na hata katika taasisi nyingine pia.

Kwa nyakati za sasa za magonjwa ya milipuko, magonjwa ya NCDs, mabadiliko ya hali ya hewa na matatizo mengine mengi ya kiafya, Afrika inahitaji kiongozi thabiti mithili ya Prof. Janabi.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akifafanua jambo.

WHO-AFRO

Afrika inahitaji kiongozi mwenye maono mapana zaidi kwa mustakabali wa vizazi vyake, CV ya Prof. Janabi inajidhirisha wazi anafaa.

Pamoja na ufanisi mkubwa unaonekana ndani ya Tanzania, nje ya Tanzania Prof. Janabi ni mshiriki wa program mbalimbali za utafiti za kimataifa.

Amefanya kazi na taasisi mbalimbali za kimataifa katika utafiti na kuboresha huduma za matibabu ya moyo.

Ni mshauri wa kimataifa (Consultant) amehudumu kama mshauri wa matibabu ya moyo kwa nchi za Kiafrika zinazotafuta msaada wa kitaalamu.

Nchi hizo ni pamoja na Malawi, Zambia, Comoro, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ni mshiriki pia wa kambi za kibingwa za kimataifa [Specialized Medical Camps].

Ameshiriki katika kambi mbalimbali za kibingwa zinazojumuisha wataalamu kutoka nchi tofauti za Afrika na kwingineko, akichangia maarifa yake ya matibabu ya moyo.

Nyadhifa hizi zimeimarisha sifa zake kama kiongozi, mshauri, na daktari mbobezi aliyetoa mchango mkubwa kwa sekta ya afya ndani na nje ya Tanzania.

Prof. Janabi amejijengea heshima kubwa kutokana na juhudi zake za kuboresha huduma za afya, maono yake ya kimkakati, na uongozi wake wa vitendo.

Hata hivyo bado WHO-AFRO haijaweka wazi utaratibu nini kitafuata ili kumpata Mkurugenzi Mkuu mpya kwani aliyepo sasa Dkt. Matshidso Moeti anaelekea kumaliza muda wake. Ni suala la kusubiri, tusubiri..

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement