moja

Responsive Advertisement


*MZRH yawafikia vijijini kwa kampeni maalum 
*Nguvu ya mwanamke yatumika kuhamasisha *Sasa wafanyiwa kisasa,wanaondoka wakiwa wamevaa suruali.

Na Veronica Mrema – Mbeya

“Kumekuwa na mwamko mkubwa, jamii sasa imeelimika, tumeweza kumfanyia tohara hadi mwanaume mwenye umri wa miaka 100,”.

Ni kauli yake Magdalena Stephen alipokuwa akinikaribisha katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH).

Magdalena ni Muuguzi Mkunga na Mtoa Huduma ya Tohara kwa Wanaume na Watoto Wachanga wenye umri kuanzia siku moja hadi 60, hospitalini hapa.

Tumefanya naye mahojiano haya maalum yanayoangazia kwa kina kuhusu tohara kwa wanaume.

Kauli yake ilinivutia na kunifanya nitamani zaidi kujua kulikoni, mwanaume huyo kukaa muda mrefu kiasi hicho pasipo kufanyiwa tohara?

“Si huyu tu, wapo wengi ambao hawakuwa wamefanyiwa tohara, tumewafanyia wakiwa katika umri mkubwa, lakini yeye ndiye mwenye umri mkubwa zaidi,” anasema.

Anasema ingawa tohara imekuwa ikifanyika kwenye jamii tangu enzi za mababu, hata hivyo imekuwa ikifanyika katika njia ambazo si salama.

“Walikuwa wakifanyiwa tohara huko porini, kwa kutumia vyombo ambavyo si salama na safi, vilikuwa havitakaswi, wakati mwingine walikuwa wakifanyiwa kundi kubwa la watu kwa kutumia kifaa kimoja.

“Hali hii ilikuwa inaweka jamii kwenye hatari zaidi kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali kama Ukimwi na magonjwa mengine ya ngono.

“Walikuwa pia hawatumii sindano ya ganzi, walikuwa wanapata maumivu makali wakati walipokuwa wakifanyiwa tohara, walipoteza kiwango kikubwa cha damu mwilini, ilikuwa hatari,” anasema.

IMANI POTOFU

Anaongeza “Licha ya kwamba tohara ilikuwa inafanyika kwenye jamii tangu kale, hata hivyo, wapo watu wengine kwenye jamii ambao hawakuwa wakifanya tohara kutokana na imani mbalimbali potofu na tafsiri ambazo si sahihi.

“Kimsingi, kwa miaka mingi mno kwenye jamii kumekuwa na uelewa duni kuhusu umuhimu wa kufanya tohara kwa mwanaume.

“Wapo pia ambao wamekuwa wakiamini kwamba mwanaume akifanyiwa tohara hupata upungufu wa nguvu za kiume na kupungua kwa ‘size’(ukubwa) wa uume, jambo ambalo si kweli.

“Walikuwa wanaamini kwamba mwanaume anapofanyiwa tohara anakatwa uume, si kweli, kinachoondolewa ni lile govi (ngozi) lililopo mbele ya kichwa cha uume, uume wenyewe hauondolewi, haukatwi.

“Wapo pia ambao walikuwa wanaamini wanaume wanaostahili kufanyiwa tohara ni waliopo kwenye dini ya uislamu pekee na dini zingine hawahusiki, si kweli,” anasema.

Anaongeza “Hawakuwa na uelewa, tohara ina manufaa mengi kwa mwanaume ikiwamo kumuepusha na maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwamo Ukimwi na mengine ya ngono.

“Mwanaume aliyefanyiwa tohara anapunguza kiwango cha kuweza kupata maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia 60,” anabainisha.

GOVI HUFICHA UCHAFU

Magdalena anasema ki-uhalisia lile govi kwa namna lilivyo huwa linaficha uchafu nakumsababishia mwanaume kutoa harufu, hata kuwa kwenye uwezekano wa kupata magonjwa ya zinaa.

“Kwa hiyo mwanaume akifanyiwa tohara anakuwa msafi, wapo ambao huofia hali ya hewa kwamba kama ni hali ya joto kidonda huchelewa kupona, lakini tohara inaweza kufanyika katika nyakati yoyote ile,” anasema.

Anasema jambo la msingi ni kuzingatia usafi wa kidonda na kwamba wanapokuwa wakitoa huduma hiyo huwa wanazingatia usiri na faragha ya mwanaume husika.

“Nimeeleza wanaume wengine wana umri mkubwa, tunazingatia maadili ya kazi, hatutoi siri ya mgonjwa, huwa tunawafanyia kuanzia wenye miaka 10 na kuendelea,” anasema.

MAANDALIZI YA KAMPENI

Anasema jitihada za kuifikia elimu zilianza tangu mwaka 2009 ambapo waliteuliwa wataalamu kwenda kupata mafunzo maalum jinsi ya kufanikisha jambo hilo.

“Ilionekana Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya Ukimwi, kwa kuangazia mambo niliyobainisha hapo awali, tuliona vema kufanya jambo la ziada kuinusuru jamii,”.

Anasema wataalamu hao waliporudi mafunzoni mara moja kampeni ilianzishwa kwa kuhakikisha wanakwenda hadi huko vijijini ili kuelimisha jamii kwa kuipatia elimu sahihi kuhusu tohara.

“Kwa kawaida huwa tunatoa huduma hapa MZRH kupitia Kitengo cha Afya ya Uzazi Meta pia tuna kituo kingine katika jingo letu lililopo huko eneo la nane nane, ambako huduma zinatolewa kila siku.

“Mteja akija tunamkaribisha vizuri, tunampa elimu sahihi na ushauri nasaha juu ya huduma tunazotoa pale kwenye kituo chetu, tunamuelekeza pia kuhusu utunzaji wa kidonda (baada ya tohara).

“Tunamueleza faida za tohara ikiwamo ile ya kumuepusha kupata maambukizi ya ukimwi kwa asilimia 60, inasaidia pia kumkinga mwanamke kutokupata maambukizi ya saratani ya kizazi,” anabainisha.

WANANDOA

“Kwa wanandoa ambao tunawafanyia upasuaji huu huwa tunawashauri baada ya tohara wasijamiiane kwa muda wa wiki sita hadi kidonda kiwe kimepona ipasavyo.

“Kwa sababu kwa ule muonekano, nje inaweza kuonesha kidonda kimepona lakini ndani kikawa bado hakijapona.

"Tunaogopa ule msuguano unaoweza kutokea wakati wa tendo, lakini ikiwa ameshindwa kabisa kuvumilia tunashauri atumie kondomu kujikinga,” anasema.

KUVAA KANGA

Magdalena anaongeza “Wapo pia wanaume ambao walikuwa wanaogopa kujitokeza kufanyiwa tohara licha ya kutangazwa kwa kampeni hiyo wakiogopa kuvaa kanga.

“Utakumbuka zamani baada ya kufanyiwa upasuaji, mwanaume kama alikuja amevaa suruali analazimika kurudi nyumbani akiwa amevaa kanda.

“Lakini mambo ni tofauti katika miaka ya sasa baada ya kuimarika kwa huduma hizi za upasuaji, tuna uwezo wa kumfanyia tohara mwanaume.

".., tukimaliza anaondoka akiwa amevaa chupi na suruali yake kama alivyokuja hospitalini,” anasema.

Anaongeza “Hatua hii imewavuta wanaume wengi kujitokeza kufanyiwa tohara, maana sasa mtu anaweza kufanyiwa na kuondoka pasipo mtu yeyote kujua kwamba fulani ametahiriwa.

NGUVU YA MWANAMKE

“Tulitumia pia nguvu ya mwanamke kufanikisha elimu hii kufika kwa jamii, tuliwaelimisha wanawake kuhusu umuhimu na faida za mwanaume kufanyiwa tohara.

“Tuliwaeleza namna tohara kwa mwanaume inavyoweza kumuepusha mwanamke kupata maambukizi ya kirusi cha HPV.

"Kirusi hiki ndicho ambacho husababisha ugonjwa wa saratani ya kizazi kwa mwanamke endapo atapata maambukizi kutoka kwa mwanaume,” anabainisha.

Anaongeza “Wanawake walipopata ile elimu walienda kuifikisha kwa waume zao, wakahamasika na kuanza kujitokeza kufanyiwa tohara, haya ni mafanikio makubwa tuliyopata kupitia kampeni hii.

TOHARA NI NINI?

Mratibu wa Huduma za Tohara kwa Wanaume MZRH, Emmanuel Nsenye anasema tohara ni upasuaji mdogo unaofanywa kwa kukata ngozi inayofunika kichwa cha uume.

“Tofauti na ile ya zamani, enzi za mababu, tohara tunayoifanya sisi wataalamu ni ya kisasa, kwanini tohara?.

"Kwa asili ya lile govi jinsi lilivyo lina seli ambazo hupitisha virusi mbalimbali kwa urahisi na hivyo kuingia katika mwili wa mwanaume,” anabainisha.

Anaongeza “Tunapomfanyia upasuaji huu, anakuwa msafi, anaepuka kupata maambukizo ya magonjwa pamoja na kumuepusha mwanamke kupata ugonjwa wa saratani ya kizazi.

“Anaepukana na tatizo la kubana kwa govi kwa mbele na nyuma kwenye uume, ni miongoni mwa faida za tohara kwa mwanaume, huduma hii tunaitoa bila malipo,” anabainisha.

WALIOFIKIWA

MZRH ilianza huduma za tohara kwa wanaume mnamo mwaka 2009, ilikuwa ndiyo the leading project mkoa wa mbeya mpaka 2014  ambapo madaraka hayo yaliachiwa kwa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.

"Tulilenga 2009 kuwafikia watu 30000, mwaka 2010 kuwafikia watu 35000, mwaka 2011 watu, mwaka 2012 watu 80000, mwaka 2013, 2014 hadi 2020 watu 100000," anabainisha.

Anaongeza "Tangu mwaka 2015 hadi sasa MZRH inajihusisha na shughuli ya tohara kwa kutoa huduma za ufundi ikiwamo kuongeza ujuzi kwa wafanya tohara wa nyanda za juu kusini kama 'mentorship'.

"Kufanya 'outreaches' za tohara kwa wanaume, kushiriki 'campaign' za kimkoa zatohara pia na za kitaifa sehemu mbali mbali za Tanzania na kufanya tohara katika static site/routine.

"Tangu mwaka 2015 hadi Sasa MZRH ilipokasimu madaraka kwa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya tayari imewafanyia tohara wanaume zaidi ya 20000," anabainisha.

MNUFAIKA

Mika Mbuja ni miongoni mwa wanaume walionufaika na huduma hii ya tohara kipitia kampeni maalum inayofanywa na wataalamu wa MZRH.

“Ni huduma rafiki, nimenufaika, nawashauri wanaume wenzangu kuchangamkia huduma hii.

"Unakuwa safi, unaepuka kupata magonjwa mbalimbali ya kuambukiza nahata kumkinga mwanamke dhidi ya saratani ya kizazi,” anatoa rai.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement