NA VERONICA MREMA – SHINYANGA
KUOKOA maisha ya mama na mtoto hasa kipindi cha kujifungua ulikuwa mtihani mzito kwa wataalamu wa afya katika Halmashauri ya Msalala iliyopo Kahama mkoani hapa.
“Wajawazito wengi walifikishwa vituo vya kutolea huduma za afya wakiwa wamechelewa, tayari wameanza kupata dalili za hatari, kwa mfano, wapo ambao tulikuta mfuko wa uzazi umeshachanika.
“Hali ilikuwa mbaya, pamoja na kufanya jitihada zote kuwasaidia, wengi wao tulijikuta tukiishia ‘ku-certify dealth’ (kuthibitisha kifo), walifariki wakati tukijitahidi kuwasaidia kujifungua,” anasema Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto, Halmashauri ya Msalala, Eva Mwanzia.
NI UTAMADUNI WA KARNE
Ni Changamoto iliyowaumiza vichwa wataalamu wa afya wa Halmashauri ya Msalala kwani jamii hasa wajawazito wenyewe hawakulipa kipaumbele suala la uzazi salama.
Hali hiyo inaelezwa kwamba ilichangia ‘kugonga mwamba’ kwa jitihada zote za wataalamu wa afya katika kumsaidia mama kujifungua na kutoka salama yeye na mwanawe.
“Ni utamaduni uliokuwapo kwenye jamii hii kwa miaka mingi, hata wanawake wenyewe hawakuona umuhimu wa kuanza mapema kiliniki ya uzazi pindi tu walipojihisi na kubainika ni wajawazito,” anasema Eva.
Anaongeza “Ndiyo maana tulikuwa tunaishia kupata vifo vingi vya uzazi ambavyo kimsingi chanzo chake kilitokana na sababu za kijamii.
MABADILIKO YA FIKRA
“Kutatua changamoto hii, ilihitajika kubadilisha mtizamo na fikra za wana-jamii, kwa kuhakikisha wanafikishiwa elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi,” anasema Mratibu wa Elimu ya Afya ya Jamii wa Halmashauri ya Msalala, Peter Ngazo.
Ngazo ambaye pia ni Mratibu wa Huduma ya Afya ya Jamii wa Halmashauri hiyo anasema waliamua kuwatumia ipasavyo watoa huduma za afya ngazi ya jamii (WAJA/ CHWs).
“Lengo letu ni kuhakikisha tunabadilisha tabia ya jamii ili iweke mtizamo chanya kutumia vituo vya kutolea huduma za afya,” anasisitiza.
MCHAKATO UPOJE?
Ngazo anasema WAJA hao huchaguliwa moja kwa moja kwenye jamii na wana jamii wenyewe.
“Kabla ya uchaguzi Halmashauri hutangaza nafasi, wanaomba, unaitishwa mkutano wa hadhara, majina yanasomwa mbele ya jamii, wanapigiwa kura, yule anayepata kura nyingi anakuwa muhudumu wao,” anabainisha.
Anasema kigezo kikuu cha kwanza kinachozingatiwa ni kuwa mkazi wa eneo husika, mwenye elimu angalau ya darasa la saba na kuendelea, elimu ya kidato cha nne huwa ni sifa ya ziada.
“Sifa hii ya ziada inampa nafasi ya kusoma kozi ya kuwa mhudumu wa afya ngazi ya jamii, katika vyuo vya serikali, ada hulipwa ama na familia, ndugu, jamaa, halmashauri au kijiji anachotoka,” anabainisha.
Anaongeza “Anapaswa asiwe na umri zaidi ya miaka 50 na sasa inashauriwa usizidi miaka 35, huwa wanazitembelea kaya moja kwa moja, hasa wale wajawazito wa mimba ya kwanza.
“Hawa huwa hawajui chochote, hawana uzoefu wowote, pia huzitembelea familia zenye watoto kuanzia mwaka sifuri hadi miaka miwili pamoja na zile familia maskini zinazohudumiwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), hawa ni walengwa wa moja kwa moja,” anabainisha.
Anasema vile vile huwatumia katika kuelimisha masuala mengi ikiwamo ya lishe, umuhimu wa chanjo, usafi wa mazingira na masuala mengineyo.
IMESAIDIA?
Eva anasema tangu Halmashauri hiyo ilipoamua kuwatumia WAJA matunda ya kazi zao yameanza kuonekana.
“Kwa mfano, tathmini tuliyofanya kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2017 hadi 2019, inaonesha idadi ya vifo vya uzazi imepungua, 2017 tulipata vifo sita, 2018 vifo saba, Januari hadi Novemba, 2019 tumepata kifo kimoja.
“Tunaona tumefanikiwa kwani hata kifo hicho kimoja kilichotokea hakikutokana na sababu ya kijamii, kilitokana na ‘complications’ ambayo mama alipata wakati tulipokuwa tukimsaidia kujifungua kwa upasuaji,” anabainisha Eva.
MAHUDHURIO YAPAA
Anaongeza “Tathmini inaonesha pia kiwango cha wanaojifungua vituoni kimeongezeka, kabla ya kuwatumia watoa huduma ngazi ya jamii kilikuwa chini ya wastani wa asilimia 60, hali ilikuwa mbaya.
“2018 takwimu zinaonesha kiwango cha waliojifungua vituoni kilikuwa asilimia 98, Januari hadi Novemba, 2019 kimeongezeka kufikia asilimia 100,” anasema.
UZAZI WA MPANGO
Eva anasema jamii haikuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya uzazi wa mpango.
“Wastani watoto ndani ya familia moja ni saba kiwango ambacho kipo juu kushinda hata kile cha Kitaifa ambacho ni watoto wanne kwa familia moja,” anasema.
Mratibu huyo anasema takwimu zinaonesha asilimia 10 pekee ya wana jamii walikuwa na uelewa kuhusu uzazi wa mpango sasa tumesogea baada ya kuwatumia WAJA asilimia 40 wanakuja kupata huduma ya uzazi wa mpango kwenye vituo vya afya.
HUTEGEMEA POSHO
Hata hivyo pamoja na kazi nzuri inayotajwa kwamba imechangiwa na juhudi zilizofanywa na WAJA katika Halmashauri hii bado wanatazamwa kama watu wanaojitolea kuisaidia jamii.
“Bado Serikali haijawaingiza rasmi kwenye mfumo wa ajira, wanafanya kwa kujitolea, huwa wanapata posho tu ambayo hutolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo tunaoshirikiana nao wakiwamo Shirika la Amref Health Africa.
“Kuna ambao walipatiwa baiskeli ili ziwasaidie katika usafiri, tunawapa posho pia kupitia makusanyo yetu kutoka chanzo kingine cha mapato (OC) ndani ya Halmashauri,” anasema Nganzo.
Anaongeza “Huwa wanapata posho kulingana na walivyofanya kazi, kwa wastani kila mmoja hutakiwa kuhudumia wa-mama 30 hadi 40 kwa kuwatembeela na kufanya marudio.
“Lakini ukijumlisha na familia nyingine unaweza kukuta ametembelea zaidi ya watu 400 kwa mwezi, kumsindikiza mzazi mmoja MJA hulipwa 8200, akitembelea kila kaya hulipwa 1250.
“Kiwango cha juu cha wastani ambacho kuna mmoja wao alipata ni kiasi cha Sh. 960,000 kikaongezeka hadi sasa amefikia Sh. milioni moja, kiwango cha chini huwa ni kati ya Sh. 400,000 hadi 200,000 ambacho mtu huweza kupata,” anasema.
SERA INAWATAMBUA?
Kipengele cha 5:1 katika Sera ya Afya Tanzania kinaelezwa mkakati wa Afya ya msingi ulilenga kuimarisha afya za wananchi kuanzia ngazi ya kaya, hadi taifa kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe.
Mkakati huu ulilenga kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu za afya kwa wananchi wote na ulitoa kipaumbele katika uboreshaji afya, kinga na tiba.
“Mwongozo unaelekeza kila kijiji kiwe na WAJA wawili na walipwe na kijiji lakini vijiji havina bajeti ya kuwalipa bado Serikali Kuu pia haijawajiriwa rasmi, wanapata posho tu.
“Tumeamua sasa hivi tunapokwenda kwenye mchakato wa bajeti tunataka kila kituo cha afya kiweke bajeti kulingana na kiwango tutakachopanga, ili wapate posho nzuri maana wanasaidia jamii,” anasema Nganzo.
KAULI YA DMO.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala (DMO), Dk. Tom Mtoi anasema hadi sasa wana jumla ya WAJA 419.
“Kweli wamesaidia mno katika kupunguza vifo vya uzazi, masuala ya chanjo, elimu ya lishe na hata kuwafuatilia kwa ukaribu wagonjwa wa Kifua Kikuu na Ukimwi ambao huacha kwenda kuchukua dawa zao vituoni,” anabainisha.
Dk. Mtoi anaongeza “Kulikuwa na mpango wa kuwaingiza ajira rasmi ya serikali, lakini ikaja hoja watatakiwa wawe kwenye ‘salary scale’ ipi, ‘parcakge’ yao itakuwa namna gani na masuala yote ya ‘security fund’, mchakato ule uliishia hivyo hadi sasa bado wanajitolea.
ITAKUWAJE?
“Mwaka wa fedha 2018/19 ili kuboresha afya ya mama na mtoto Halmashauri ilitenga kiasi cha Sh 12 (asilimia tatu) na kiasi cha Sh. milioni nne (asilimia moja) zilitengwa kwa ajili ya posho ya WAJA, lakini bahati mbaya posho hiyo haikutoka hadi sasa,” anabainisha Nganzo.
Diwani wa Kata ya Ikinda, Matrida Msoma anasema ni vema kuanza kusimamia kwa dhati kuhakikisha fedha hizo zilizotengwa zinapatikana kwa wakati.
“Watu hawa wanasaidia jamii, wanafanya kazi kubwa na nzuri, tunaona vifo vya uzazi vilivyopungua, tulishakubaliana kutenga fedha hiyo, wataalamu wetu waandike dokezo kuziomba, vinginevyo tutakuwa hatuwatengei haki,” anasema.
Diwani wa Kata ya Mwarugulu, Flora Sagasaga anashauri Idara ya Afya kuona umuhimu wa kutetea fedha hizo zitoke kwa wakati ili watoa huduma za afya ngazi ya jamii wapate maslahi yao.
“Wanahangaika kusaidia jamii, lakini wanapata wapi maslahi,? Lazima tujiulize, tumekubaliana kutenga fedha lakini hazitoki, kwanini?,” anahoji.
Anaongeza “Ingawa bajeti yenyewe bado ni ndogo lakini ni muhimu sasa kamati ya fedha wakafuatilia jambo hili kwa ukaribu, wakumbushie kwenye vikao vyao.
Naye, Diwani wa Kata ya Ngaya, Mchui Simbila anasema pamoja na kwamba WAJA hupata posho kutoka Mfuko wa RBF na kupitia wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwamo AMREF Health Afrika, ni muhimu pia Halmashauri hiyo kujidhatiti.
“Tuanze kujiuliza mradi utakapofungwa na wafadhili kuondoka WAJA watawezeshwa na nani,? Wanafanya kazi kubwa lakini kwanini iwe kwa hisani? Ni vema Halmashauri ijipange iwalipe lakini si kwa hisani,” anashauri.
Anaongeza “Tunaweza kuamua na kupanga kima cha chini kiwe kiasi gani tuanze kuwalipa, watu hawa wana faida kwetu, haiwezekani wasilipwe, kwanini tusiwatambue?.
“Ili wawe ‘committed’ maana wakati mwingine unakuta mtu anaamka usiku wa manane kwenda kumsaidia mama, wanafanya kazi ya msingi mno… hatuwatendei.
“Pamoja na kwamba bado Serikali Kuu haijawaingiza kwenye mfumo rasmi wa ajira, lakini lazima tukubaliane kubeba mzigo huu wa kuwalipa, wajue kabisa wanalipwa kiasi gani, posho iwe ya ziada, kuwapa motisho,” anashauri.
Chapisha Maoni