KUNA watu huwa hawana desturi ya kuugua mara kwa mara, tofauti na wengine ambao maradhi kwao ni kawaida.
Ili kuepuka maradhi ya mara kwa mara, kuna mambo mengi ambayo binadamu anapaswa kuyazingatia.
Leo tutazungumzia siri nane ambazo watu wasiougua mara kwa mara huzingatia.
1. Pata mapumziko ya kutosha
Matokeo ya tafiti nyingi zilizofanyika katika sehemu mbalimbali duniani yanaonyesha kwamba, watu wanaopata usingizi wa kutosha huwa na furaha na afya bora.
Tafiti zinaonyesha kwamba kupumzika na kupata usingizi kwa saa nane na zaidi ni muhimu katika kudumisha afya, kuzuia magonjwa na kukupa furaha.
Kukosa usingizi na kutokupata mapumziko ya kutosha huchangia kupandisha kiasi cha homoni zinazosababisha msongo wa mawazo na matatizo chungu nzima ya kiafya.
2. Fanya mazoezi

Mazoezi yana faida lukuki, ikiwa ni pamoja na kuzuia magonjwa sugu kama vile kisukari na magonjwa ya moyo. Mazoezi pia huongeza kinga ya mwili na kuongeza kiwango cha homoni zinazoleta hali ya furaha mwilini.
3. Epuka unywaji pombe kupindukia

Watu wenye uwezo wa kudhibiti kiasi cha kilevi wanachotumia hufurahia vinywaji wavipendavyo huku wakizilinda afya zao.
Ikumbukwe kwamba, kiwango cha pombe kinachokubalika kiafya, kwa watu wengi huweza kuonekana ni kidogo hivyo kuwafanya kunywa kupindukia. Unywaji pombe kupita kiasi huweza kusababisha madhara mengi kwa afya na hata kuhatarisha maisha yetu.
4. Jali unachokula

Chakula kinaweza kuwa dawa au sumu kwa maana ya kiasi na aina ya chakula. Kula chakula bora ni kitu muhimu katika kudumisha afya bora.
Matokeo ya tafiti yanaonyesha kwamba watu wanaojali wanachokula kwa kuzingatia kula chakula bora hujikinga na aina nyingi za magonjwa hivyo kuwa na afya bora na furaha tele.
5. Kuwa na mitazamo chanya
Huchagua ubora juu ya kiasi na kuto jilinganisha au kujishindanisha na watu wengine.
6. Cheka mara kwa mara
Ziko tafiti nyingi zinazoonyesha umuhimu wa kutabasamu na kucheka katika kudumisha afya. Watu wanaotabasamu na kucheka mara kwa mara hujikinga na msongo wa mawazo hivyo kukaribisha furaha na afya katika maisha yao.
Tafiti zinaonyesha pia kwamba, watu hawa huishi maisha marefu yaliyojawa na afya na furaha.
7. Lala na kuamka mapema
Kulala kwa muda wa kutosha peke yake haitoshi. Tafiti zinaonyesha kwamba, kulala mapema na kuamka mapema ni muhimu katika kudumisha afya na kuleta furaha maishani.
Baada ya kufanya kazi wakati wa mchana, kwa kawaida miili huwa imechoke hivyo
kuhitaji mapumziko. Lakini pia huwa na nguvu na ufanisi mkubwa wakati wa alfajiri.
Kwa maana hiyo, ni muhimu kulala mapema ili angalau kutimiza saa nane.
8. Nawa mikono mara kwa mara

Tabia ya kunawa mikono mara kwa mara husaidia kuzuia magonjwa mbalimbali.
Matokeo ya tafiti hizo yanaonyesha kwamba kunawa kwa kutumia sabuni hutukinga na magonjwa kama vile kuharisha, mafua na magonjwa ya tumbo.
Ziko tafiti zilizowafuatilia watu wenye tabia ya kunawa mara kwa mara na kuwalinganisha na wale wasio na tabia hiyo na kubaini kwamba wenye tabia ya kunawa mikono mara kwa mara huwa na kinga ya magonjwa ya mlipuko kwa asilimia mpaka tisini.
Wataalamu na wanasayansi wanatushauri kunawa kabla na baada ya kula chochote, pia kunawa tunapotoka msalani na hata tunapotoka sehemu zenye mikusanyiko ya watu.
Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa mtandao wa Jamii Health.
Chapisha Maoni