moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Dawa ni nguzo muhimu katika mfumo wa huduma za afya. Hata hivyo, ubora wa dawa pekee hauwezi kuhakikisha mgonjwa anapata matokeo bora ya matibabu.

Kinachojenga mfumo imara wa huduma za famasi ni uwepo wa wataalamu wenye sifa, usimamizi madhubuti wa vituo vinavyotoa huduma za dawa, mifumo ya udhibiti inayofanya kazi kwa ufanisi na uzingatiaji wa sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya famasi.

Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imeendelea kuimarisha mfumo huo kupitia maboresho mbalimbali yaliyolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za famasi, kusimamia ubora wa wataalamu na kuhakikisha dawa zinatolewa katika maeneo yaliyoidhinishwa na salama kwa matumizi ya wananchi.

Takwimu za Baraza la Famasi zinaonesha, sekta ya famasi nchini Tanzania imekua kwa kiwango kikubwa kati ya mwaka 2015 na 2026. 

Idadi ya wanataaluma waliosajiliwa imeongezeka kutoka 1,264 mwaka 2015 hadi 4,494 mwaka 2026. Vile vile idadi ya maduka ya dawa yaliyosajiliwa imeongezeka kutoka 1,116 hadi 11,245.

Ukuaji huo umeonekana pia kwa wataalamu wa kada mbalimbali. Idadi ya wafamasia imeongezeka kutoka 677 hadi 3,792, huku mafundi dawa sanifu idadi yao imeongezeka kutoka 1,250 hadi 16,087. 

Vyuo vinavyotoa mafunzo ya famasi vilivyoidhinishwa navyo vimeongezeka kutoka 519 hadi 1,190, wakati mafundi dawa wasaidizi wameongezeka kutoka watatu hadi sita.

Kwa mujibu wa Msajili wa Baraza la Famasi, Mfamasia Magige, mabadiliko hayo ni matokeo ya juhudi zinazoendelea za Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma za dawa na usimamizi wa taaluma ya famasi.

Anasema moja ya hatua muhimu zilizochangia mafanikio hayo ni kuanzishwa kwa Ofisi za Kanda sita za Baraza la Famasi zinazohudumia Kanda ya Kaskazini, Ziwa, Mashariki, Nyanda za Juu Kusini, Kati na Magharibi.

Anasema ofisi hizo zimeongeza ufanisi katika usajili wa wataalamu, ukaguzi wa vituo vya huduma za dawa, usimamizi wa utekelezaji wa sheria na kanuni pamoja na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wadau waliokuwa wakilazimika kufuata huduma makao makuu.

Mbali na kuimarisha usimamizi kupitia ugatuzi wa huduma, Baraza limeendelea kutumia teknolojia katika utoaji wa huduma zake. 

Mifumo ya usajili kwa njia ya kielektroniki, malipo ya kidijitali na programu ya simu ya mkononi imeboresha upatikanaji wa huduma kwa wataalamu wa famasi na wananchi.

Mfamasia Magige anasema matumizi ya teknolojia yamepunguza urasimu, yameongeza uwazi katika utoaji wa huduma na kurahisisha upatikanaji wa taarifa kuhusu wataalamu waliosajiliwa pamoja na vituo vinavyoruhusiwa kutoa huduma za dawa.

Katika kuhakikisha ukuaji wa sekta unaendana na ubora wa wataalamu, Baraza linaendelea kushirikiana na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania [TCU] kuboresha programu za mafunzo ya famasi.

Ushirikiano huo unalenga kuhakikisha mitaala inakidhi mahitaji ya sasa ya sekta ya afya na kwamba wahitimu wanakuwa na ujuzi wa kutoa huduma salama na zenye ubora.

Mbali na kusimamia wataalamu, Baraza lina jukumu la kusajili na kukagua maeneo yote yanayotoa huduma za dawa, ikiwemo famasi za jumla, famasi za rejareja na Maduka ya Dawa Muhimu [DLDM]. 

Lengo ni kuhakikisha dawa zinatolewa katika mazingira yanayokidhi viwango vya kitaaluma na kisheria.

Baraza linasimamia maadili ya wanataaluma kupitia Kanuni ya Utendaji [Code of Practice] na Kanuni ya Maadili ya Wanataaluma wa Famasi. 

Kanuni hizo zinawaelekeza wataalamu kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na kwa kuzingatia usalama wa wagonjwa.

"Katika kusimamia ubora wa huduma za dawa nchini, Baraza linaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba [TMDA] ili kuhakikisha dawa zinazowafikia wananchi zinakidhi viwango vya ubora, usalama na ufanisi," anasema.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, matumizi sahihi ya dawa yanaendelea kuwa jukumu la pamoja kati ya wataalamu wa afya na wananchi. 

Matumizi holela ya dawa yanaweza kusababisha usugu wa vimelea dhidi ya dawa, kuongeza gharama za matibabu na kuhatarisha afya ya mgonjwa. 

Kwa mujibu wa World Health Organization, usugu wa vimelea dhidi ya dawa [Antimicrobial Resistance - AMR] ni miongoni mwa vitisho vikubwa zaidi vya afya ya umma duniani. 

Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa mwaka 2019 takribani watu milioni 1.27 walifariki dunia moja kwa moja kutokana na maambukizi yaliyosababishwa na vimelea vilivyokuwa sugu kwa dawa, huku vifo vinavyohusishwa na usugu huo vikifikia milioni 4.95. 

WHO inaeleza kuwa matumizi yasiyo sahihi ya antibiotiki, kujitibu bila ushauri wa mtaalamu, kutomaliza dozi na matumizi holela ya dawa katika binadamu na mifugo ni baadhi ya sababu kuu zinazochochea tatizo hilo. 

Hali hiyo imeifanya Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine, kuendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa dawa na kuhamasisha matumizi sahihi ya antibiotiki ili kupunguza kasi ya kuongezeka kwa usugu wa vimelea.

Mfamasia Magige anasisitiza "Wananchi wanapaswa kupata dawa kutoka katika vituo vilivyosajiliwa na kutumia dawa kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.

".., ili kuongeza ufanisi wa matibabu, kupunguza madhara yanayoweza kuzuilika na kulinda uwezo wa dawa kuendelea kutibu magonjwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo".

Kadiri sekta ya afya inavyoendelea kukua, huduma za famasi nazo zinaendelea kuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha wananchi wanapata dawa salama, huduma bora na ushauri sahihi wa matumizi ya dawa. 

Ukuaji wa idadi ya wataalamu, vituo vya huduma na matumizi ya teknolojia unaonesha hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha mfumo wa dawa nchini.

Kadhalika, changamoto zilizopo zikihitaji ushirikiano endelevu kati ya serikali, wataalamu wa afya, sekta binafsi na wananchi ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za famasi zenye ubora, salama na zinazokidhi viwango vya kitaaluma.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement