Kila kitu katika maisha ya Prinu Joseph na mumewe Dinish Antony kilionekana kuwa cha kawaida kabisa.
Aliishi maisha yenye uwiano na afya nzuri, akifanya mazoezi mara kwa mara, kula chakula chenye lishe, na kuepuka pombe, sigara, pamoja na vyakula vya haraka.
“Kwa hivyo, kila kitu kilikuwa kawaida sana sana,” alikumbuka kwa tabasamu tulivu. “Hadi siku moja, mnamo Novemba 2024, nilipokuwa nikijichunguza.”
Ilikuwa siku ya kawaida, lakini kile alichogundua kilibadilisha kila kitu. “Mara nyingi mimi hufanya ukaguzi wa matiti yangu wakati wa kuoga,” alieleza.
“Siku hiyo, nilihisi uvimbe mdogo sana katika titi langu moja, si hata kwamba ni uvimbe mkubwa mno, ilikuwa uvimbe mdogo sana.
Sikuwa na wasiwasi mkubwa sana katika hatua hiyo, Siku iliyofuata, nikaangalia tena, bado niliuhisi.”
Shauku yake ikageuka kuwa wasiwasi. “Niliomba mume wangu aangalie naye pasipo kumuambia kile nilichokihisi, alikagua matiti yote mawili.
"Alipofanya hivyo, naye alihisi ule uvimbe mdogo mno katika titi langu la upande wa kulia." Anasema anakumbuka hiyo ilikuwa Novemba 22, tarehe ambayo hakuna mmoja wao ambaye ataisahau.
Hadi wakati huo, Prinu hakuwa na dalili yoyote, hakuna maumivu, na hakuwa na historia ya familia ya saratani ya matiti.
“Hakuna jamaa wetu aliyewahi kupata saratani ya matiti,” anasema. “Hata daktari alinihoji zaidi kujua kama kuna kitu/kiashiria ambacho kinaweza kutiliwa shaka huenda ndiyo sababu ya mimi kuugua.
Anaongeza “Nilianza kupata hedhi yangu nikifika miaka 14, niliolewa nikiwa na miaka 24, na nilipata watoto wangu wawili kabla ya kufikisha miaka 29.
"Hata hivyo, bado nilikutwa na ugonjwa huu. Sasa hii ilinifanya nitambue kwamba mtu yeyote anaweza kupata saratani.”
Mume wake, Antony, anakubali kwa kimtazamo, akiwa kando yake wakati wa mahojiano haya maalum anasema. “Yeye [Prinu] alikuwa anazingatia mtindo bora wa maisha na alikuwa na afya nzuri kabla.
“Hapendi kuvuta sigara, hapendi pombe, hula vyakula vyenye sukari nyingi au vya haraka, lakini bado alipata saratani.
"Hapo ndipo nilipoelewa kwamba ugonjwa huu unaweza kumgusa mtu yeyote na akaugua," anasema.
Siku ya Uchunguzi
Kwa mgonjwa wa saratani yeyote, Prinu anasema kwa upole, “Siku ya kwanza unapoambiwa unaugua saratani ni siku ngumu sana, si rahisi kupokea majibu hayo.
Antony anaongeza, “Ni jambo zito lakini shida kubwa zaidi inaweza kutokea ikiwa mgonjwa husika anayepewa habari yako, atakapoipokea kwa mtizamo hasi.
"[Unajua sisi] wengine tunaweza kumpa usaidizi, lakini hatima nzima unayo wewe [kwa sababu] ndiye unayebeba mzigo [wa tatizo husika].
Anasisitiza "Prinu ni mtu mwenye nguvu na alipokea kwa mtizamo chanya sana. Alikuwa tayari anafahamu kuhusu saratani ya matiti na uelewa.
"Kwamba ukilinganisha na saratani nyingine, saratani ya matiti ni mojawapo ya zinazotibika zaidi, ikiwa mtu anawahi kufanya uchunguzi wa awali na kupata matibabu ya mapema.”
Wanandoa hao, ingawa walipata mshtuko mdogo kutokana na ripoti hiyo ya uchunguzi wa maabara, lakini walipata faraja kubwa kwamba itatibiwa na kupona.
“Kwa kuwa hakuwa na dalili au matatizo mengine ya kiafya, tuliamini ilikuwa hatua ya kwanza,” Antony alieleza. “Tulikuwa na imani kwamba matibabu ya kitabibu yangefanikisha.”
SAFARI YA IMANI
Kupata matibabu hakukuwa rahisi, lakini hawakuwa peke yao. “Tuna mfumo wa usaidizi wa ajabu kila upande wetu,” Antony anabainisha na kuongeza..,
“Watoto wetu wawili, wazazi wetu, ndugu na dada wote walituzunguka tangu siku ya kwanza.”
Kipindi wanandoa hao waliamua kusafiri hadi India kwa uchunguzi zaidi, familia zao tayari zilikuwa hatua moja mbele.
“Dada yake, ambaye anaishi Dubai, alifika India siku moja kabla yetu. Wazazi wake na wazazi wangu tayari walikuwa pale,” Antony anaeleza.
“Tulikuwa na marafiki wakitupa ukaguzi kila wakati. Ilionekana kama tumezungukwa na upendo pande zote,” alitabasamu.
Siku walipowasili India mapema aliafanyiwa uchunguzi zaidi, alipewa ushauri na matibabu kuanza mapema.
Prinu anasema "Tulijua tayari ilikuwa saratani, lakini tulikuwa tunasubiri kusikia aina na hatua yake.”
Siku hiyo hiyo, walipokea matokeo. “Ilikuwa hatua ya mwanzo [stage moja one] na tulikubali,” Antony anasisitiza.
“Tulibarikiwa kuwa na mmoja wa madaktari bora wa upasuaji wa matiti, na tulijihisi salama.” Licha ya dhoruba ya hisia, mahitaji ya vitendo yaliwasaidia kubaki imara.
“Unapojishughulisha na kupanga safari, kuhudhuria miadi ya matibabu, na kujiandaa kwa upasuaji, huna muda mwingi wa kuzama katika hofu,” Prinu anasema.
Anaongeza “Kuwa na msaada thabiti kutoka kila upande kunabadilisha maisha kabisa.”
Antony anahimiza tena jambo muhimu. “Unaweza kuwa na mfumo bora zaidi wa msaada [wa tiba] familia, marafiki, jamii lakini kama mgonjwa ana mtizamo hasi/dhaifu ndani, kila kitu kinaanguka.
"Prinu muda mwingi alikuwa mwenye tabasamu hata baada ya upasuaji. Madaktari hawakuamini!.” anasema Antony.
'NGUVU YA NDANI'
Prinu alipitia upasuaji mkubwa wa aina mbili: upasuaji wa kuondoa matiti (mastectomy) na upasuaji wa kuondoa kizazi na mayai (hysterectomy) ili kumkinga mbali zaidi dhidi ya saratani hiyo.
Hata hivyo, asubuhi baada ya upasuaji, daktari wake alishangaa, anasema. “Alipokuja chumbani kwangu, alisema, ‘Una hakika niliondoa matiti yako kweli?
"Kwa sababu unaonekana kama hujapitia upasuaji mkubwa wa aina mbili tofauti!’” Prinu alitabasamu muda wote. Nguvu yake tulivu iliwashangaza wote waliomzunguka.
Antony anadokeza "Ilikuwa mojawapo ya wakati wa kuhamasisha zaidi maishani mwangu.
“Alikuwa akitabasamu, ameketi, akizungumza kama hakuna kilichotokea. Hapo ndipo nilipoelewa kweli ni jinsi gani alikuwa na ujasiri mkubwa,".
MAISHA BAADA YA TIBA
kwa walio wengi, saratani imebadili kila kitu katika mwili, hisia na hata vipaumbele vyao. Ndivyo ilivyo pia kwa Prinu anakumbuka, “Mnamo Novemba uliopita, nilikuwa tofauti kabisa kiafya.
“Sasa, mwili wangu umebadilika kwa '365 digrii' [anamaanisha kwa kiwango kikubwa] . Lakini nilijifunza kujipenda tena na tena, kukubali kila alama kama sehemu ya uhai wangu.”
Anasisitiza “Watu wengi wanaogopa uchunguzi, wanafikiri ["Nikifanya kipimo, kama nitapata kitu kibaya?’ Hofu hiyo inawazuia kupata msaada mapema.
"Lakini mara tu unaposhinda hofu hiyo, safari inakuwa rahisi sana. Sehemu ngumu zaidi ni kuchukua hatua ya kwanza," anasema.
UPENDO UNAOSHINDA ALAMA
Swali: Mniwie radhi kwa kuuliza jambo hili, lakini nimeshuhudia ndoa nyingi zikivunjika baada ya mama kuathiriwa na saratani hii, je kwako imekuwaje?
Prinu anatabasamu na kusema "Bila samahani, tena umeniuliza swali zuri. Awali hata mimi niliogopa na kuhofia hilo pia na nilikuwa najiuliza sana ndani yangu," anakiri na kuongeza,
"[Hata baada ya upasuaji] 'mastectomy', nilikuwa na wasiwasi kama mume wangu bado angenitazama vivyo hivyo na kunipenda. Nilimuuliza pia.”
Antony anapokea swali hilo na kusema "Nilimwambia, ["Sasa nakupenda zaidi kuliko kabla"] wote wanatabasamu.
Anaongeza “Kwa sababu ya yote aliyopitia na jinsi tulivyopigana pamoja, ninathamini zaidi. Upendo wetu haukubadilika, umeimarika.”
“[Nilimwambia, vipi kama] kungetokea jambo kwangu, labda ningepoteza miguu yangu au kuungua je, ningeweza kutegemea angeondoka? Upendo wa kweli haukimbii.
“Mnakuwa pamoja, iwe ni kipindi cha maumivu na ugonjwa. Tatizo la dunia ya leo ni kwamba upendo umepungua, wengi hubadilika mara moja. Lakini unapompenda kweli mtu, unabaki naye bila shaka.”
Prinu anatabasamu tena “Hakika, ninahisi kupendwa zaidi sasa, mume wangu ananilinda na anaonesha mapenzi zaidi, ananathamini zaidi, najiona mwanamke mwenye bahati kubwa duniani.
“Namshukuru sana mume wangu, familia yangu, jamii yangu na kila mtu aliye nami. Nafikiri mgonjwa yeyote aliye na mfumo thabiti wa msaada anaweza kushinda kila kitu," anasisitiza.
UJUMBE KWA WANAUME
Antony anawapa wanaume ujumbe wenye nguvu. “Hii si tu kuhusu saratani,” anasema kwa uthabiti na kusisitiza.
“Ikiwa unampenda mtu basi lazima uwe naye katika safari yote. Usiondoke na kumtelekeza peke yake wakati mambo yanapokuwa magumu.”
Anaongeza “Ukiondoka kwa mpendwa wako na kumuacha peke yake, jaribu kujiuliza vipi ingekuwa mgonjwa huyo ni wewe mwenyewe.
"Na wakati itatokea, wengine wakaondoka?! Kila kitu unachokitenda ujue pia kinaweza kukuletea baraka au kinyume chake. Hivyo, kama unampenda mtu, kuwa naye kabisa.”
UJASIRI MKUU
Ni wanandoa pekee waliombatana pamoja katika Pink Picnic ambayo iliandaliwa na Shujaa Cancer Foundation [SCF] na kufanyika Oktoba 14, 2025 huko Msasani Beach.
Tukio la kipekee linalolenga kuelimisha jamii kuhusu saratani ya matiti ambayo ni miongoni mwa saratani zenye idadi kubwa ya wagonjwa duniani na Tanzania pia.
Saratani hiyo inaongoza namba moja na huchangia vifo vya mamilioni ya watu kila mwaka duniani.
Kisa cha Prinu na Antony kilikuwa na msisimko wa kipekee kwa kila aliyefika katika Pink Picnic hiyo ndipo M24 TANZANIA MEDIA ikafanya nao mahojiano haya maalum ili kufikia jamii pana zaidi.
Ni hadithi ya ukumbusho mahususi kwamba uchunguzi wa awali husaidia kwa kiwango kikubwa kuokoa uhai.
“Ugonjwa wa saratani hauathiri tu mwili wako, huathiri pia akili, imani na hata mahusiano, lakini leo nina ujasiri mkubwa baada ya matibabu ya mapema, nimepona,” Prinu anasema.
Kauli yake ambayo inaweka msisitizo wa kuhimiza jamii kufanya uchunguzi wa mapema kama vile inavyoshauriwa na madaktari bingwa wa magonjwa ya saratani duniani.





Chapisha Maoni