moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Kisa cha mwanamke mwenye umri mdogo ambaye aligundulika na saratani ya matiti, u kwenye matibabu ya ki-bingwa kwa mwaka mmoja sasa, kinagusa mioyo ya wengi.

Ndani ya ukumbi mdogo ulipo kwenye makazi ya Balozi wa Sweden nchini Tanzania,  macho yangu yanashuhudia Balozi Charlotta Ozaki Macias akichukua ‘tishu’ mezani kwake na kufuta machozi.

Tupo zaidi ya wanawake 20 ndani ya ukumbi huu, tumefika kwa mwaliko wa Balozi Charlotta ikiwa ni mwezi mahususi wa uelimishaji jamii kuhusu saratani hiyo, ‘Pink October’.

Balozi Charlotta ndiye mgeni rasmi anayezindua semina hii ya siku moja, aliyoalika pia Shujaa Cancer Foundation ili kuwaelimisha wafanyakazi wa ubalozi, kuna waliotoka balozi nyingine kadhaa pia.

Kila meza aliipatia ‘assignment’ “Naomba kabla sijazindua, msalimiane, mjadiliane kidogo kwa nini mmekuja hapa na unatarajia kujifunza nini?.

Hapo ndipo ilipotoka simulizi fupi ya kisa cha Emilly Bavu, mwanamke mdogo anayepambana na saratani ya matiti.

Emily alijenga desturi ya kuchunguza matiti yake kufuatia kifo cha mama yake mzazi aliyekutwa na ugonjwa huo pia.

Miezi kadhaa kupita tangu kifo cha mama yake alibaini tofauti ndogo katika titi lake la kushoto.

Baadae iligundulika naye ana saratani ya matiti na kuanza matibabu ni miaka miwili sasa akipatibiwa [makala haya tutakueletea kwa ukubwa na undani wake, siku zijazo].

Simulizi ya leo ni ya Balozi Charlotta, mahojiano maalum na M24 TANZANIA MEDIA, karibu ufuatane nasi...

“Unajua kwanini nimelia, naelewa anachokipitia. Mimi pia niliugua saratani ya matiti, nikiwa Sweden .., ni safari ngumu,” anasema.

Anaongeza “Miaka 10 iliyopita, nikiwa na umri wa miaka 4 na mama wa wasichana warembo wawili [wadogo], nilipogundulika nina saratani ya matiti.

Ni jambo lililomshtua kwa sababu mtindo wake wa maisha ulikuwa mzuri namna ile inavyoshauriwa na wataalamu wa masuala ya afya, alijiweka mbali na vihatarishi vinavyoweza kusababisha saratani.

“[Ukweli] sikuamini kama mimi ningepata saratani ya matiti. Nilidhani labda [anastahili kuugua] mtu mwingine, lakini si mimi,” anasimulia kwa utulivu.

NINI KILITOKEA?

Alianza kuhisi maumivu katika matiti yangu na mikononi, alidhani labda ni kwa vile alitumia muda mwingi kufanya kazi kwa ‘kompyuta’ yake.

Anasimulia zaidi, “Niliamua kwenda kuonana na mtaalamu wa mazoezi tiba (physiotherapist). Lakini  mtaalamu huyo alinituma kwa daktari kwa uchunguzi zaidi.

“Baada ya kufanyiwa [uchunguzi kwa kipimo cha] mammografia, matokeo yalionesha nilikuwa na uvimbe mkubwa wa sentimita 5.5.

“Hapo ikawa mwanzo wa safari yangu ngumu, ya matibabu dhidi ya saratani,” anasimulia Balozi Charlotta na kuongeza,

“[Yaani] ghafla [maisha yalibadilika], nilijikuta nikianza safari iliyodumu takribani mwaka mmoja, nikiwa kwenye tiba ya kemikali (chemotherapy), upasuaji na mionzi (radiotherapy)”.

Anasema safari hiyo haikuwa rahisi, kwani alipitia changamoto nyingi ikiwamo kushuka kwa kinga mwilini, maambukizi ya mara kwa mara na uchovu mkubwa.

“Wakati huo huo, nilikuwa na jukumu la kulea watoto wangu wadogo, lakini nilikuwa na bahati.

“.., kwa sababu nchini Sweden tuna mfumo mzuri wa afya unaofadhiliwa na Serikali. Sikulazimika kulipa gharama za matibabu.

“Pia nilipatiwa likizo ya ugonjwa bila kupoteza mshahara wangu wote. Kwa hiyo nililindwa ki-fedha [uchumi] na nikaweza kuzingatia matibabu,” anasema.

UCHUNGUZI MAPEMA

Somo kubwa la kujifunza katika visa vyote viwili [cha Emilly na Balozi Charlotta] ni kwamba elimu kuhusu saratani ni muhimu kumfikia kila mmoja.

Uchunguzi wa mapema pia ni jambo la msingi kulizingatia, Balozi Charlotta anasisitiza “Nimeeleza kwamba sikuwahi kufikiria kama ningekuwa miongoni mwa waliougua saratani.

“[Kwa sababu] nilikuwa mlaji mzuri wa mbogamboga kwa miaka mingi, nafanya yoga na michezo mingine pia, sivuti sigara na pombe nilikuwa nakunywa kiasi kidogo mno.

“Pia sina historia ya mtu aliyewahi kuugua saratani yoyote ile katika familia ya baba na mama yangu, kwa hiyo nilidhani niko salama.

“Lakini, nilipougua nilijifunza somo muhimu; saratani inaweza kumtokea mtu yeyote, hata yule mwenye mtindo bora wa maisha na asiye na historia ya ugonjwa huu kwenye familia yake,” anasema.

SHAHIDI ZA KI-SAYANSI

Ni hoja inayoungwa mkono pia na shahidi nyingi za ki-sayansi zilizofanyika kwa miaka mingi hadi sasa duniani.

Asilimia 90 ya watu wanaougua magonjwa ya saratani ikiwamo hiyo ya matiti hawakuwahi kuwa na historia ya ugonjwa huo ndani ya familia zao.

Ni 10% tu ya wagonjwa wote duniani ambao wana historia ya kuwahi kupata mgonjwa wa saratani katika familia zao.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Shaban Juma anasema pamoja na hayo, kuna vihatarishi vinavyoweza kuchangia mtu kupata magonjwa ya saratani.

“Kuna sababu zisizoweza kubadilika ikiwamo za urithi wa vinasaba, kupata hedhi katika umri mdogo, kuchelewa kukoma hedhi, kuwa na msongamano mkubwa wa ‘tishu’ katika matiti,

“Kuna sababu zinazoweza kubadilishwa kama vile uzito kupita kiasi, unywaji wa pombe, ukosefu wa mazoezi, na matumizi ya homoni baada ya kukoma hedhi.

Anaongeza “Shirika la Afya Duniani (WHO) sasa linabainisha wazi kuwa hakuna kiwango salama cha unywaji pombe, likisisitiza umuhimu wa kuzingatia mtindo bora wa maisha.

Kwa upande mwingine, wataalamu wanasema kuwa kuwa na watoto na kunyonyesha mara kwa mara hupunguza hatari ya kupata saratani ya matiti.

Kwa sababu kipindi cha kunyonyesha humpa mwili mapumziko kutokana na homoni ambazo zinahusiana na mzunguko wa hedhi.

Hata hivyo, kuchelewa kupata mtoto zaidi ya umri wa miaka 30 huongeza hatari. Licha ya saratani hii kuhusishwa zaidi na wanawake, wanaume nao huugua, ingawa ni kwa 1%.

MATIBABU HUTOFAUTIANA

Si kila mgonjwa hupewa matibabu ya aina moja, hutofautiana kati ya mmoja na mwingine.

Dkt. Juma anafafanua zaidi, “Matibabu hutegemea aina ya saratani [aliyonayo mgonjwa husika] na yanaweza kujumuisha upasuaji, chemotherapy, tiba ya homoni au tiba ya mionzi.

Anasema Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine yanayoendelea, inazidi kuchukua hatua katika kupambana na magonjwa ya saratani.

“Kwa kupitia elimu kwa umma, kuimarisha huduma za afya ngazi ya msingi ili kusogeza uchunguzi wa mapema karibu zaidi na jamii, upatikanaji wa huduma bora matibabu pia,” anasema.

Anaongeza “Lakini ni muhimu kujua pia uhai wa mgonjwa hauishii baada ya matibabu, wengine hukumbwa na changamoto za kimwili, kisaikolojia, na kijamii.

“Hivyo, msaada wa familia na jamii ni muhimu katika safari ya uponyaji. Elimu ni silaha kubwa,” anasema na kuongeza,

“Utambuzi wa mapema unaokoa maisha, kila mmoja awe balozi wa elimu ya saratani  ili kuokoa maisha ya wengi zaidi,” anasisitiza Dkt Juma.

BALOZI NA TANZANIA

“Ongezeko la muda wa kuishi [life expectancy] kwa watu wa Tanzania limechangia pia kuongezeka kwa visa vya saratani,” anasema Balozi Charlotta.

Anaongeza “Watu wanaishi muda mrefu zaidi, na kadri miaka inavyoongezeka [kwa mujibu wa shahidi za ki-sayansi], ndivyo uwezekano wa kupata saratani unavyoongezeka.

“Hivyo Watanzania wanahitaji kujifunza zaidi kuhusu namna ya kuishi kwa afya bora lishe, mazoezi pamoja na kuzingatia uchunguzi wa mapema,” anashauri.

Anasisitiza ni muhimu wanawake na wasichana vijana kufahamu miili yao, hasa kupitia kuchunguza binafsi matiti yao mara kwa mara.

“Pia kwena hospitalini, kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi kwa kipimo cha mammografia kadri umri unavyoongezeka,” anashauri.

SWEDEN & TANZANIA

Kwa upande wa ushirikiano wa kimataifa, anasema Serikali ya Sweden imekuwa bega kwa bega na Tanzania kwa zaidi ya miaka 60 katika kuboresha huduma za afya.

“Tulisaidia sana wakati wa mapambano dhidi ya UKIMWI na tumeendelea kushirikiana katika kuboresha huduma za msingi za afya,” anabainisha.

Balozi Charlotta anaongeza “Sasa tunasaidia zaidi katika kuelimisha jamii kupitia matukio kama haya na kushirikiana na taasisi kama Shujaa Cancer Foundation pamoja na Wizara ya Afya.

“Pia tunasaidia kampuni ya ki-Sweden inayotengeneza vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa saratani ya matiti (mammography), ili teknolojia hiyo ipatikane si tu mijini bali pia vijijini”.

TUVUNJE UNYANYAPAA

Pamoja na hayo, anasisitiza elimu ni jambo la msingi kulizingatia kwa nguvu kubwa kwa sababu ni ngao kubwa dhidi ya saratani.

“Tunahitaji kuzungumza wazi wazi kuhusu saratani kama tunavyoongelea shinikizo la damu au kisukari.

“Haitokani na kurogwa na waganga wa kienyeji wala si laana. Hii ni changamoto ya hali ya ki-afya ambayo inaweza kumpata mtu yeyote.

Anaongeza “Miaka 100 iliyopita, 90% ya wanawake waliougua saratani ya matiti walifariki dunia, lakini sasa hali imebadilika 90% wanatibiwa na kupona, wanaishi.

“Tafiti na sayansi zimepiga hatua kubwa. Ni lazima tubaki na matumaini,” anasema Balozi Charlotta

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement